Msimamo wa Marekani unaokinzana na wa dunia kuhusu mgogoro wa Libya
-
Mapigano baina ya pande hasimu mjini Tripoli, Libya
Mapigano mapya yaliyoanzishwa na Jenerali Khalifa Haftar anayeungwa mkono na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri huko Libya umeifanya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika irejee katika ajenda muhimu za kisiasa duniani huku kukiwa na mitazamo tofauti kuhusu namna ya kuutatua mgogoro huo.
Katika hali ambayo nchi nyingine za Ulaya bado zinaiunga mkono serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Waziri Mkuu Fayez al Sarraj ambayo inatambuliwa pia na Umoja wa Mataifa, rais wa Marekani, Donald Trump alisema katika mahojiano aliyofanyiwa siku ya Jumatatu kuwa amezungumza na Jenerali Khalifa Haftar, mkuu wa wapiganaji wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya ikiwa ni katika kumuunga mkono jenerali huyo.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, White House amewaambia waandishi wa habari kuwa, katika mazungumzo ya simu baina ya rais wa Marekani na Jenerali Khalifa Haftar, Trump alimpongeza jenerali huyo kwa nafasi yake nzuri katika kile alichosema ni kupambana na ugaidi na kulinda usalama wa visima vya mafuta vya Libya. Vile vile wawili hao walijadiliana mitazamo yao ya pamoja kuhusu njia za kuleta utulivu na kuunda utawala wa kisiasa na kidemokrasia nchini Libya.
Mazungumzo ya simu baina ya rais wa Marekani na Jenerali Khalifa Haftar wa Libya yamefanyika katika hali ambayo, kama tulivyosema, jamii ya kimataifa inaitambua serikali ya Umoja wa Kitaifa ya mjini Tripoli kuwa ndiyo serikali halali nchini Libya.
Mtaalamu mmoja wa masuala ya kisiasa, Nadia al Bilbasi amesema, mazungumzo ya simu yaliyofanyika baina ya Trump na Khalifa Haftar ni mabadiliko mapya ambayo yanakinzana kikamilifu na matamshi ya viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ya wiki za hivi karibuni.
Mazungumzo hayo ya simu ya Trump na Jenerali Khalifa Haftar yanaweza kuhesabiwa kuwa ni kubadilisha Washington msimamo wake na kudhihirisha kwa uwazi zaidi siasa za Marekani za kushadidisha mgogoro na machafuko nchini Libya.
Wiki mbili nyuma, Marekani iliondoa nchini Libya wanajeshi wake wapatano 200 katika hali ambayo nchi za Ulaya kama vile Italia bado zinaendelea kushikilia msimamo wao wa kuiunga mkono serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Waziri Mkuu Fayez al Sarraj zikisisitizia haja ya kuongezwa juhudi za kisiasa za kuleta mapatano na kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi huru wa kidemokrasia nchini Libya.
Enzo Moavero Milanesi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia amesema: hakuna njia yoyote ya kijeshi inayoweza kutatua masuala mazito na nyeti ya kisiasa nchini Libya.
Mapigano makali yanaendelea hivi sasa nchini Libya huku Jenerali Khalifa Haftar aliye na baraka kamili za waitifaki wake kama Misri, Imarati na Saudia ambazo zinammiminia misaada mingi ya kifedha, ndiye aliyeanzisha mapigano mapya ya kujaribu kuuteka mji mkuu Tripoli kwa tamaa ya kuiungusha serikali ya Umoja wa Kitaifa inayotambuliwa rasmi kimataifsa. Hata hivyo muqawama wa majeshi ya serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa na kuingia mikono mingine ya nje katika masuala ya Libya kwa mara nyingine yamevuruga mlingano wa kisiasa wa nchi hiyo.
Ghassan Salamé, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ametahadharisha kuhusu wimbi kubwa la silaha zinazomiminwa nchini Libya hivi sasa na kuzidi kuwa mbaya hali ya kiusalama ya nchi hiyo. Amesema, hali ya kibinadamu ni mbaya mno nchini Libya na hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana katika mchakato wa kisiasa wa nchi hiyo.
Naam, mgogoro mpya ulioanzishwa na Jenerali Khalifa Haftar anayeungwa mkono na rais wa Marekani Donald Trump na vibaraka wake kama Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri, umevuruga juhudi zote za kisiasa na mbali na kuleta matatizo mengi ya kiuchumi, unatishia pia kuundwa serikali ya kidikteta na kibaraka nchini Libya.
Kwa upande wake, jamii ya kimataifa imekumbwa na wasiwasi mkubwa kuhusu Libya katika hali ambayo hitilafu zilizopo nje ya Libya kuhusu njia za kuutatua mgogoro wa nchi hiyo zinazidi kuchochea moto huku wahanga wakuu wakiendelea kuwa raia wa kawaida wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.