Katiba mpya ya Misri na mustakabali wa nchi hiyo
(last modified Thu, 25 Apr 2019 02:21:11 GMT )
Apr 25, 2019 02:21 UTC
  • Katiba mpya ya Misri na mustakabali wa nchi hiyo

Asilimia 88.8 ya wananchi wa Misri walioshiriki katika kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba ya nmchi hiyo wamepiga kura ya ndiyo na kwa muktadha huo, Rais Abdulfattah as-Sisi wa nchi hiyo anaweza kuendelea kutawala hadi mwaka 2030.

Suala la marekebisho ya Katiba nchini Misri kwa muda mrefu  lilikuwa ni changamoto kwa jamii ya kisiasa ya Misri. Hatimaye baada ya Bunge la Misri kupasisha suala la kuweko marekebisho hayo, kura ya maoni ya marekebisho ya Katiba imefanyika nchini Misri. Hata hivyo, takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Misri zinaonyesha kuwa, ushiriki wa kura hiyo ya maoni  ulikuwa mdogo ambapo ni asilimia 44.33 tu ya wananchi wa nchi hiyo waliotimiza masharti ya kupiga kura ndio walioshiriki katika kura hiyo ya maoni.

Kufanyiwa marekebisho kipengee cha 140 cha katiba hiyo, sasa kipindi cha urais wa nchi hiyo kimerefushwa kutoka miaka 4 hadi 6. Kwa msingi huo, Rais wa nchi ataiongoza Misri kwa duru mbili za miaka sita sita badala ya duru mbili za miaka minne minne ya hapo awali. Mbali na kurefushwa kipindi cha urais, Seneti ya nchi hiyo iliyofutwa mwaka 2011 kufuatia malalamiko ya wananchi dhidi ya dikteta Husni Mubarak imehuishwa tena, rais amepewa mamlaka makubwa ya kuwateua majaji na wanawake wamepewa asilimia 25 ya viti vya bunge.

Awali akthari ya wananchi na wapinzani wa serikali walipinga vikali kufanyiwa marekebisho katiba hiyo wakisema kuwa lengo la serikali ni kuendelea kumbakisha madarakani Abdulfattah al-Sisi. Abdulfattah as-Sisi aliingia madarakani baada ya kumpindua kijeshi Rais Muhammad Mursi mwaka 2013. Katika kipindi hicho as-Sisi alikuwa Waziri wa Ulinzi. Alihodhi madaraka ya nchi hiyo baada ya kuandaa uchaguzi wa kimaonyesho mwaka uliofuata wa 2014. Tokea wakati huo hadi sasa as-Sisi amekuwa akitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa kuwakandamiza wapinzani wa serikali kutokana na uungaji mkono mkubwa anaopata kutoka kwa nchi za Magharibi hususan Marekani.

Rais Abdulfattah al-Sisi wa Misri

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, marekebisho ya katiba yaliyofanyika nchini Misri kupitia kura ya maoni ni hatua ya ukandamizaji yenye lengo la kuimarisha mfumo unaotawala katika nchi hiyo.

Kundi jingine la wakosoaji wa marekebisho ya Katiba nchini Misri linaamini kwamba, marekebisho hayo yana lengo la kuongeza nguvu na mamlaka ya jeshi la nchi hiyo. Kwa mtazamo wao ni kuwa, marekebisho yaliyofanyika yanandaa uwanja wa uwezekano wa jeshi kuwa na nguvu na ushawishi zaidi katika siasa za Misri. Muhammad al-Baradei, mwanasiasa na mwadiplomasia mkongwe wa Misri sambamba na kukosoa marekebisho ya katiba nchini Misri amesema kuwa, marekebisho hayo ni batili na ni kurejea nyuma mwamko wa mageuzi katika nchi za Kiarabu.

Uingiliaji wa madola ya kigeni na taathira yake katika siasa za Misri ni jambalo nalo limewatia wasiwasi mkubwa wapinzani wa marekebisho ya katiba ya nchi hiyo. Kwa uoni wao ni kuwa, msukumo wa kurefusha muda wa kuweko madarakani Rais Abdulfattah al-Sisi unapaswa kuchunguzwa nje ya nchi hiyo na katika manufaa ya utawala haramu wa Israel pamoja na washirika wake wa Kiarabu na kieneo. Kimsingi ni kuwa, wakosoaji hawa wanaamini kuwa, kabla ya marekebisho haya ya katiba kuwa ni hitajio la ndani, ni matokeo ya uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Maandamano dhidi ya serikali nchini Misri

Muhammad Sudan, Katibu wa Mahusiano ya kigeni ya Chama cha Uhuru na Uadilifu cha Misri yeye anaamini kuwa, kufanyia marekebisho katiba ya Misri na kurefusha kipindi cha uongozi wa Rais Abdulfattah al-Sisi kumefanyika katika fremu ya  malengo ya Washington na Tel Aviv kwa minajili ya kuzikalia kwa mabavu ardhi zote za Palestina.

Mkabala na hilo, waungaji mkono wa marekebisho ya katiba ya Misri na wafuasi wa Abdulfattah al-Sisi wao wanaamini kwamba, mabadiliko hayo yana udharura kwani, yanampa muda zaidi Rais huyo wa kukamilisha mipango na miradi yake mikubwa ya ujenzi na kusukuma mbele gurudumu la ustawi wa uchumi. Aidha wanaashiria hatari kubwa ya ugaidi na ukosefu wa uthabiti hususan mgogoro wa Libya wakisema kuwa, ili kuivusha Misri katika mazingira haya, nchi hiyo inahitajia serikali yenye nguvu na ndio maana wanataka Rais Abdulfattah al-Sisi aendelee kuiongoza nchi hiyo.

Inaonekana kuwa, kufanyika marekebisho ya katiba nchini Misri kumeifanya nchi hiyo iingie katika kipindi kipya katika uga wa kisiasa, kipindi ambacho endapo viongozi wa Cairo wataghafilika, basi huo unaweza kuwa mwisho wa matunda ya mapinduzi ya nchi hiyo na kufutiliwa mbali juhudi za kufikia demokrasia na mamlaka ya kujitawala nchini humo.

Tags