Kodivaa kuongeza idadi ya askari wake wa kulinda amani nchini Mali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53120-kodivaa_kuongeza_idadi_ya_askari_wake_wa_kulinda_amani_nchini_mali
Rais wa Ivory Coast ametangaza kuwa nchi yake itatuma mamia ya askari zaidi kwenda kujiunga na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali (MINUSMA).
(last modified 2025-10-20T07:03:11+00:00 )
Apr 27, 2019 07:42 UTC
  • Kodivaa kuongeza idadi ya askari wake wa kulinda amani nchini Mali

Rais wa Ivory Coast ametangaza kuwa nchi yake itatuma mamia ya askari zaidi kwenda kujiunga na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali (MINUSMA).

Alassane Ouattara aliyasema hayo jana Ijumaa na kufafanua kuwa, Kodivaa itatuma askari 650 kwenda kujiunga na wenzao 150 nchini Mali, na hivyo kuifanya nchi hiyo iwe moja ya wachangiaji wakubwa wa wanajeshi wa MINUSMA.

Katika kikao na waandishi wa habari, Rais Outtara amesema, "Lazima tuimarishe ushirikiano wetu wa kiusalama sambamba na kufanya jitihada za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Libya ambao umechangia pakubwa ukosefu wa usalama katika nchi jirani zetu kama Niger, Mali, Burkina Faso na nyinginezo."

Haya yanaripotiwa wiki moja baada ya watu wenye silaha kuua askari wasiopungua 10 wa jeshi la Mali baada ya kushambulia kambi moja ya jeshi hilo katika eneo la Guire katikati mwa nchi.

Wanajeshi wa MINUSMA wakilinda doria

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres alitahadharisha kwamba, hali ya kiusalama nchini Mali inazidi kuwa mbaya kutokana na kuongezeka mashambulizi ya kigaidi dhidi ya askari wa kimataifa wa kulinda amani na wanajeshi wa serikali.

Kikosi hicho cha MINUSMA kina askari 12,500 ambao walitumwa nchini Mali mwaka 2013 kwa ajili ya kuwadhaminia usalama raia, lakini vikosi hivyo havijakuwa na utendaji wa kuridhisha katika kurejesha utulivu huku vitisho vya ugaidi vikiendelea kuitatiza nchi hiyo.

Hadi sasa askari karibu 200 wa MINUSMA wameuawa wakiwa kazini.