Larijan: Iran na Nigeria kuimarisha ushirikiano wao wa kibiashara
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53298-larijan_iran_na_nigeria_kuimarisha_ushirikiano_wao_wa_kibiashara
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema mazingira yameandaliwa kwa ajili ya kuimarisha na kupanua ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Nigeria katika uga wa biashara.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 05, 2019 23:16 UTC
  • Larijan: Iran na Nigeria kuimarisha ushirikiano wao wa kibiashara

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema mazingira yameandaliwa kwa ajili ya kuimarisha na kupanua ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Nigeria katika uga wa biashara.

Ali Larijani alisema hayo jana Jumapili katika mazungumzo yake na mjumbe wa Bunge la Wawakilishi la Nigeria hapa mjini Tehran na kubainisha kuwa, "Hakuna mpaka wowote ulioko wa kufanya biashara na Nigeria, na wawekazaji wa nchi hiyo wako huru kufanya biashara katika soko la Iran."

Dakta Larijani amesisitiza kuwa, miradi ya madini nchini Nigeria ni moja ya sekta zinazohitaji mashirika na wafanyabiashara wa Iran kwa ajili ya kubadilishana mawazo na kufanya biashara na wenzao wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Kadhalika Spika wa Bunge la Iran ameashiria kuhusu mikakati inayofanywa na serikali ya Tehran kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wake na Abuja katika nyuga za matibabu, nishati, elimu na biashara ya magari.

Emmanuel Ibe Kachikwu, Waziri wa Mafuta wa Nigeria

Aprili 26, Emmanuel Ibe Kachikwu, Waziri wa Mafuta wa Nigeria ambayo ni mwanachama wa Shirika la Nchi Zinazouza Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) alitoa radiamali kufuatia uamuzi wa Marekani wa kufuta kibali cha ununuzi wa mafuta ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa, ni jambo lisilowezekana kufikisha mauzo ya mafuta ya Iran kwenye kiwango cha sifuri, na kwamba kwa vyovyote vile, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuuza mafuta yake. 

Tarehe 22 mwezi uliopita wa Aprili 2019, serikali ya Marekani ilitangaza kuwa, haitoongeza muda wa msamaha wa kununua mafuta ya Iran kwa wanunuzi wakuu wa bidhaa hiyo muhimu.