"Wafanyakazi wa viwanda vya nguo Ethiopia ndio wenye mshahara mdogo zaidi duniani"
Ripoti mpya imefichua kuwa, wafanyakazi wa viwanda vya ufumaji nguo nchini Ethiopia ndio wanaolipwa mshahara mdogo zaidi duniani.
Utafiti uliofanywa na Kituo cha Biashara na Haki za Binadamu cha Chuo Kikuu cha New York umeonesha kuwa, wanaofanya kazi katika viwanda hivyo vya ufumaji nguo nchini Ethiopia wanalipwa mshahara wa dola 26 za Marekani kwa mwezi, mshahara ambao ni mdogo zaidi ukilinganisha na wa wafanyakazi wengine wa viwanda hivyo katika nchi mbalimbali duniani.
Waandishi wa ripoti hiyo, Paul M. Barrett na Dorothée Baumann-Pauly wamesema, "hatua ya serikali ya Addis Ababa ya kujaribu kuvutia wawekezaji ajinabi katika sekta hiyo imechangia pakubwa wafanyakazi hao wa viwanda vya ufumaji nguo kulipwa mshahara huo wa chini nchini Ethiopia."
Wamesema hii ni licha ya Ethiopia kuwa moja ya chumi zinazokuwa kwa kasi kubwa barani Afrika. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, aghalabu ya wafanyakazi hao wanashindwa kukidhi mahitaji yao na familia zao kutokana na mshahara huo mdogo.
Ripoti hiyo imetoa mfano ikisema wafanyakazi wa viwanda vya kufuma nguo nchini Kenya wanalipwa dola 207 kwa mwezi, huku China ikiwalipa wafanyakazi wake katika sekta hiyo mshahara wa dola 340.
Kituo cha Biashara na Haki za Binadamu cha Chuo Kikuu cha New York kilitumia katika utafiti wake kiwanda cha Hawassa Industrial Park kilichofunguliwa na serikali Juni mwaka 2017, chenye wafanyakazi 25,000 ambao mara kwa mara wamekuwa wakifanya migomo, huku baadhi yao wakichoshwa na kuacha kazi.