Jeshi la Nigeria lawafyatulia risasi hai waandamanaji wanaotaka kuachiwa Sheikh Zakzaky
Watu kadhaa wamejeruhiwa baada ya jeshi la Nigeria kuwafyatulia risasi hai waandamanaji wanaotaka kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiliwe huru.
Duru za habari zinaarifu kuwa, maandamano hayo yalifanyika usiku wa kuamkia leo na kwamba waandamanaji kadhaa wanauguza majeraha ya risasi.
Waandamanaji hao walisikika wakipiga nara ya kutaka kuachiwa huru kiongozi huyo wa Kiislamu nchini humo, ambaye anazuiliwa kwa miaka minne sasa na vyombo vya usalama vya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Mapema mwezi huu, timu ya madaktari iliyomfanyia uchunguzi wa kiafya Sheikh Zakzaky, ambaye tokea alipotiwa mbaroni na kushikiliwa kizuizini mwaka 2015, hajawahi kufanyiwa uchunguzi wa kitiba, ilisema mwanachuoni huyo anahitaji matibabu ya dharura nje ya nchi.
Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walipigwa risasi na baadaye kukamatwa na kuwekwa kizuizini tarehe 13 Desemba 2015, wakati askari wa jeshi la Nigeria walipovamia na kufanya hujuma dhidi ya Hussainiyyah ya mji wa Zaria katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa nchi hiyo.
Mnamo mwezi Desemba 2016, Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa hukumu ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiwe huru mara moja, sambamba na kulitaka jeshi na vyombo vya usalama viilipe familia yake fidia ya dola laki moja na nusu, lakini si tu vimekaidi kutekeleza hukumu hiyo ya mahakama lakini vimeendelea pia kumweka kizuizini kiongozi huyo wa kidini pamoja na mkewe.