Basi jingine la watalii lashambuliwa karibu na Mapiramidi ya Giza, Misri
Watu 16 wamejeruhiwa katika shambulizi la bomu lililolenga basi la watalii karibu na Mapiramidi ya Giza, eneo ambalo ni kivutio kikuu cha watalii, nje kidogo ya mji mkuu wa Misri, Cairo.
Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, bomu lililokuwa limetangwa karibu na uzio wa Makavazi Kuu ya Misri liliripuka wakati basi hilo la watalii lilipokaribia uzio huo, yapata kilomita 2 kutoka Mapiramidi ya Giza.
Habari zaidi zinasema kuwa, aghalabu ya waliojeruhiwa katika hujuma hiyo ni watalii na kwamba baadhi yao wako katika hali mahututi. Hakuna habari yoyote ya kifo iliyoripotiwa kutokana na shambulizi hilo.
Mwishoni mwa mwaka uliopita, watalii watatu wa Vietnam na raia mmoja wa Misri waliuawa baada ya bomu lililotegwa kando ya barabara kuripukia basi lililokuwa likifanya safari ya kitalii karibu na Mapiramidi ya Giza. Basi hilo lilikuwa limebeba watu 16 wakiwemo watalii 14.
Katika kulipiza kisasi, maafisa usalama wa Misri waliripotiwa kuwaua watu 40 wanaotuhumiwa kuhusika na shambulizi hilo la kigaidi.
Misri kwa muda mrefu sasa imekuwa ikishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi yenye silaha dhidi ya raia na pia wanajeshi na maafisa usalama wa serikali.