Kenya yasema haina mvutano wa kidiplomasia na Somalia
Serikali ya Kenya imekanusha tetesi kuwa kuna mvutano wa kidiplomasia na nchi jirani ya Somalia.
Katibu wa Kudumu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya Macharia Kamau amewaambia waandishi habari jijini Nairobi kuwa, Kenya daima imekuwa ikiwahudumia raia wa Somalia wanaoishi nchini Kenya. Aidha amesema Somalia inatakiwa kuheshimu mamlaka ya ardhi ya Kenya huku nchi hiyo nayo ikiwa inaheshimu mahitaji kadhaa ambayo inapaswa kuyapa Somalia.
Mapema wiki hii, maofisa watatu wa serikali ya Somalia wakiwa na hati za kusafiria za kidiplomasia walizuiwa kuingia nchini Kenya kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.
Kamau amesema, tukio hilo halimaanishi kuwa kuna uhusiano mbaya kati ya nchi hizo mbili, bali ni suala la idara ya uhamiaji. Katika tukio hilo waziri na maseneta wawili wa Somalia walizuiwa kuingia Nairobi kwa ajli ya shughuli rasmi na hatimaye wakilazimika kurejea Mogadishu.
Serikali ya Somalia imelalamikia rasmi hatua hiyo ya maofisa wake wa kidplomasia kuzuiwa kuingia nchini Kenya. Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia imesema kuzuiwa maofisa wake kuingia Nairobi ni jambo ambalo limekiuka ujirani mwema baina ya Somalia na Kenya na kutahadharisha kuwa vitendo kama hivyo vinaweza kuvuruga uhusiano mzuri wa pande mbili.
Hayo yanajiri wakati ambao nchi hizo bado zinazozana kuhusu eneo la mpaka katika Bahari ya Hindi baada ya kuibuka taarifa kuwa Somalia ilikuwa imepiga mnanda maeneo yenye utajiri wa mafuta katika eneo linalozozoaniwa baina ya nchi mbili.
Swala hilo liliwasilishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu ICJ mnamo mwezi Aprili 2014 na linaendelea kusikilizwa.
Pamoja na kuwepo mzozo huo askari wa Kenya wanaendelea kuhudumu Somalia kuisaidia seriakli ya nchi hiyo kukabiliana na magaidi wa Al Shabab na kurejesha amani nchini humo.