Mahakama ya Kenya yaamuru wahajiri 22 wa Eritrea warudishwe kwao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53708-mahakama_ya_kenya_yaamuru_wahajiri_22_wa_eritrea_warudishwe_kwao
Mahakama nchini Kenya imeagiza raia 22 wa Eritrea waliokamatwa siku 10 zilizopita na kushtakiwa kwa kuwa nchini humo kinyume cha sheria warejeshwe nchini kwao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 25, 2019 03:46 UTC
  • Mahakama ya Kenya yaamuru wahajiri 22 wa Eritrea warudishwe kwao

Mahakama nchini Kenya imeagiza raia 22 wa Eritrea waliokamatwa siku 10 zilizopita na kushtakiwa kwa kuwa nchini humo kinyume cha sheria warejeshwe nchini kwao.

Hakimu Kennedy Cheruiyot jana Ijumaa alifahamishwa kuwa washukiwa hao waliingizwa nchini kupitia magendo ya binadamu, wakiwa na nia ya kusafiri hadi Afrika Kusini kusaka ajira. 

Washtakiwa hao waliojumuisha wanawake 12 walimsihi Hakimu Cheruiyot aamuru warudishwe kwao licha ya changamoto wanazokumbana nazo nchini humo.

Akisoma agizo hilo, Cheruiyot alisema, “Naamuru washtakiwa wakabidhiwe ubalozi wao nchini ndipo warudishwe nchini kwao. Washukiwa wamekaa rumande kwa muda mrefu na haki zao zimekandamizwa."

Wakizugumza kupitia mkalimani, washtakiwa hao walisema walitoroka nchini kwao kwa sababu ya dhiki mbalimbali na ukosefu wa ajira na walikuwa wanaenda Afrika Kusini kujitafutia riziki.

Ramani ya Eritrea

Washtakiwa hao walikiri mbele ya mahakama kuwa walikamatwa mnamo Mei 15 mwaka huu 2019, wakiwa nchini Kenya kinyume cha sheria za uhamiaji. 

Maafisa wa serikali ya Kenya wanasema mpaka mrefu baina ya Kenya na Ethiopia katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ndio sababu kuu ambayo huwawezesha wafanya magendo ya kusafirisha binadamu kutumia njia hiyo kuwasafirisha wahamiaji haramu.