Magaidi wa Al Shabab wahujumu kituo cha jeshi la Somalia
Kundi la kigaidi la Al Shabab limeshambulia kituo cha jeshi la Somalia katika eneo la kusini mwa nchi hiyo ambapo watu kadhaa wamejeruhiwa.
Kwa mujibu wa taarifa hujuma hiyo imejiri katika eneo la Bilis Qooqaaani ambalo liko nje ya mji wa Afmadow katika jimbo la Lower Juba kusini mwa Somalia.
Kwa mujibu wa taarifa, katika hujuma hiyo kumejiri ufatulinaji risasi baina ya magaidi wakufurishaji wa Al Shabab na askari wa serikali ya jimbo hilo. Mapigano yaliendelea hadi pale askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika (AMISOM) walipofika katika eneo na kuhitimisha hali hiyo. Askari wa Somalia na pia wapiganaji wa kundi la Al Shabab walijeruhiwa katika mapigano hayo.
Wanajeshi wa serikali ya Somalia wakishirikiana na askari wa kikosi cha Umoja wa Afrika maarufu kama AMISOM wameimarisha vita dhidi ya magaidi wakufurishaji wa al-Shabab katika maeneo ya kati na kusini mwa Somalia ambapo wamefanikiwa kuwaangamiza magaidi wengi.
Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 na katika miaka ya hivi hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wakufurishaji wa Al Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.
Wakati huo huo , Waziri wa ulinzi wa Somalia Hassan Ali Mohamed jana amekipongeza kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kwa juhudi zake kwenye kurejesha amani na usalama nchini humo.
Ali Mohamed alisema hayo mjini Mogadishu alipohutubia hafla ya kusherehekea Siku ya Afrika. Amesema lengo moja la kuanzisha Umoja wa Afrika ni kutoa mchango katika operesheni za kulinda amani barani Afrika, na AMISON ni mfano mzuri wa manufaa ya Umoja wa Afrika. Ameipongeza tume hiyo kwa kazi zake katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miongo kadhaa nchini Somalia, ambavyo vimeiharibu nchi hiyo na kuwafanya wananchi wake wakimbie makwao.
Amesisitiza kuwa nchi za Afrika lazima zitatue suala la wakimbizi, ili kusaidia kuwazuia vijana wa Afrika kukimbilia Ulaya.