HRW: Misri imetenda jinai za kivita katika mkoa wa Sinai
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Righs Watch (HRW) limesema kuwa askari usalama wa Misri wametenda jinai za kivita kwa kuwalenga kwa mashambulizi raia katika Peninsula ya Sinai kaskazini mwaMisri.
HRW imeeleza kuwa jeshi na polisi ya Misri katika Peninsula ya Sinai nchini humo linatenda jinai kubwa na ukandamizaji dhidi ya raia. HRW imebainisha hayo kupitia ripoti yake yenye kurasa 134 iliyoitoa leo Jumanne.
Shirika hilo limesema kuwa baadhi ya ukandamizaji huo ambao jeshi na askari usalama wa Misri wanatuhumiwa kuutenda unatajwa kuwa sawa na jinai za kivita. Ripoti hiyo ya HRW ilifanyiwa utafiti kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka jana 2018; huku ripoti hiyo ikiwa imewashirikisha wakazi, wanaharakati, waandishi habari na mashahidi wengine wa Sinai kaskazini zaidi ya 50 wakiwemo maafisa wa zamani wa serikali, jeshi na picha za satalaiti.
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu (HRW) limelituhumu jeshi la Misri kwa kuwatia mbaroni watu kwa umati, kupoteza watu kwa lazima, kutesa, mauaji ya kiholela na kuendesha mashambulizi ya anga na ya nchi kavu dhidi ya raia kinyume cha sheria.