Polisi ya Nigeria yakosolewa kwa kuwashambulia waandamanaji Siku ya Quds
Polisi ya Nigeria imekosolewa vikali kwa kuwashambuliwa Waislamu na wanaharakati walioshiriki matembezi ya amani ya Siku ya Kimataifa ya Quds jana Ijumaa.
Ibrahim Mousa, msemaji wa kitengo cha habari cha Harakati ya Kiislamu Nigeria amesema watu kadhaa wamejeruhiwa huku wengine wengi wakitiwa mbaroni na maafisa usalama kwa kushiriki maandamano hayo ya Siku ya Quds yaliyofanyika katika barabara za jimbo la Kaduna, katikati mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Amekosoa vikali kitendo cha maafisa usalama kuwafyatulia waandamanaji hao mabomu ya gesi ya kutoa machozi na risasi hai, badala ya kuwapa ulinzi wananchi hao waliokuwa wakishiriki matembezi ya amani.
Kadhalika waandamanaji hao walitumia jukwaa hilo kushinikiza kuachiliwa huru haraka iwezekanavyo, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe zinazosema "Uhuru kwa Palestina" na "Uhuru kwa Zakzaky". Sheikh Zakzaky anazuiliwa na vyombo vya usalama vya Nigeria tokea Disemba mwaka 2015, baada ya wanajeshi wa Nigeria kuivamia Husainia ya mji wa Zaria na kuwaua kiholela Waislamu hao ikiwa ni pamoja na kuwapiga risasi Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe.
Nigeria hapo jana ilijiunga na nchi nyingine duniani hususan za Kiislamu katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds, kuonyesha uungaji mkono wao kwa wananchi madhulumu wa Palestina, ambao kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakifanyiwa kila aina ya ukatili na utawala wa Kizayuni wa Israel.