5 wauawa baada ya maafisa usalama kushambulia waandamanaji Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53889-5_wauawa_baada_ya_maafisa_usalama_kushambulia_waandamanaji_sudan
Habari kutoka Khartoum, mji mkuu wa Sudan zinaarifu kuwa, kwa akali watu watano wameuawa baada ya maafisa usalama nchini humo kushambulia kwa risasi hai maandamano ya wananchi wanaolalamikia hatua ya jeshi la nchi hiyo kung'ang'ania madaraka.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jun 03, 2019 02:44 UTC
  • 5 wauawa baada ya maafisa usalama kushambulia waandamanaji Sudan

Habari kutoka Khartoum, mji mkuu wa Sudan zinaarifu kuwa, kwa akali watu watano wameuawa baada ya maafisa usalama nchini humo kushambulia kwa risasi hai maandamano ya wananchi wanaolalamikia hatua ya jeshi la nchi hiyo kung'ang'ania madaraka.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa, makabaliano hayo kati ya waandamanaji wanaotaka kuundwa serikali ya kiraia na maafisa usalama yamefanyika mapema leo Jumatatu nje ya makao makuu ya jeshi katika mji mkuu Khartoum.

Waandamanaji hao wenye ghadhabu wamefunga barabara zote muhimu mjini Khartoum, huku wakiapa kuendelea kukita kambi nje ya makao makuu hayo ya jeshi licha ya kushambuliwa kwa risasi hai na mabomu ya kutoa machozi.

Jana Jumapili pia, polisi na jeshi la nchi  hiyo waliwashambulia kwa risasi wananchi walioendeleza maandamano na kukusanyika mbele ya Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo katika mji mkuu Khartoum na kumuua kijana mmoja wa miaka 20 na kujeruhi wengine 10.

Baraza la Kijeshi la Mpito linaloongoza Sudan hivi sasa

Makundi ya mawili yanayoongoza maandamano hao ya raia nchini Sudan, yaani Jumuiya ya Wanataaluma wa Sudan na "Muungano wa Makundi ya Ukombozi na Mabadiliko" ambao ndio muungano mkubwa zaidi wa wapinzani huko Sudan yametoa taarifa tofauti na kulaani hatua ya jeshi la Sudan ya kuwashambulia kwa risasi waandamanaji, kufanya mauaji, kuwagonga kwa magari na kuwapiga marungu raia wanaoandamana kwa amani yakisisitiza kuwa, lengo la wanajeshi hao wa Sudan lilikuwa ni kuua.

Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan limeonya kuhusu kuundwa serikali ya kiraia nchini humo hivi sasa na kudai kuwa, jambo hilo litazidisha machafuko nchini humo.