Askari 8 wa serikali wauawa Sinai Misri
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imetangaza habari ya kuuawa askari wanane wa serikali katika mkoa wa Sinai wa kaskazini mwa nchi hiyo.
Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imetangaza habari hiyo na kunukuu taarifa iliyotolewa leo na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri ikisema kuwa, askari wanane wa nchi hiyo wameuawa katika shambulizi la magaidi kwenye mji wa al Arish mkoani Sinai.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imesema pia kuwa magaidi watano wameuawa katika mapigano hayo.
Mapigano huwa yanatokea mara kwa mara baina ya magenge ya kigaidi na jeshi la Misri katika mkoa wa Sinai wa kaskazini mwa nchi hiyo na katika baadhi ya maeneo mengine ya Misri.
Machafuko yameongezeka nchini Misri katika miaka ya hivi karibuni hasa baada ya jeshi kufanya mapinduzi mwaka 2013 yaliyomuondoa madarakani Mohammed Morsi rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo. Tangu wakati huo mashambulizi ya kigaidi yameendelea huku wananchi wakionesha kutoridhishwa na jinsi serikali inavyoshindwa kulinda usalama wao.
Mwezi uliopita wa Mei, jeshi la Misri lilitangaza kuwa limeua magaidi 47 wenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh katika operesheni ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo kwenye mkoa wa Sinai Kaskazini.
Msemaji wa jeshi la Misri, Tamer al-Rifai alisema kuwa, makumi ya magaidi wenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh wameangamizwa katika eneo la Sinai Kaskazini kufuatia operesheni ya siku kadhaa ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo.