Askari wa AMISOM Somalia wagawa chakula siku kuu ya Idul Fitr
Kikosi cha kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kimesema askari wake wameimarisha shughuli za kibinadamu zinazolenga kuboresha maisha ya Wasomali.
Ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku Kuu ya Idul Fitr baada ya mfungo wa mwezi wa Ramadhani, askari wa AMISOM wamegawa chakula na dawa katika maeneo kadhaa nchini humo.
Kwa mnasaba wa Idul Fitr, mkuu wa AMISOM Francisco Madeira ametuma salamu za heri na fanaka kwa seriakli na watu wa Somalia. Amesema askari wa AMISOM wanajiunga na Waislamu wa Somalia katika sherehe za Idul Fitr. Aidha amewapongeza maafisa wa usalama wa Somalia kwa kudumisha amani katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Kati ya maeneo ambayo AMISOM imegawa chakula ni kwa wakimbizi mjini Dhobley katika eneo la Lower Juba. Zoezi hilo limesimamiwa na kamanda wa kada ya pili ya AMISOM Brigedia Jenerali Dickson Ruto.
Wakati huo huo Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limeonya kuhusu kuongezeka kwa Wasomali wanaokimbia maafa ya ukame nchini kwao ambako watu zaidi ya milioni 2 wanahitaji msaada wa chakula.
Shirika hilo limetoa wito wa misaada ya dharura ya ziada ili kuwasaidia watu walioathirika na kukimbia maafa ya ukame nchini Somalia, ambapo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu milioni 5.4 wanakadiriwa kukabiliwa na uhaba wa chakula kuanzia Julai, na watu milioni 2.2 kati yao watahitaji msaada wa dharura.
Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 na katika miaka ya hivi hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wakufurishaji wa Al Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.