Watu kadhaa wauawa katika kampeni ya uasi wa kiraia Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54029-watu_kadhaa_wauawa_katika_kampeni_ya_uasi_wa_kiraia_sudan
Kwa akali watu wanne wameripotiwa kuuawa na maafisa usalama katika kampeni ya uasi wa kiraia wa nchi nzima iliyoanza jana Jumapili nchini Sudan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 10, 2019 03:17 UTC
  • Watu kadhaa wauawa katika kampeni ya uasi wa kiraia Sudan

Kwa akali watu wanne wameripotiwa kuuawa na maafisa usalama katika kampeni ya uasi wa kiraia wa nchi nzima iliyoanza jana Jumapili nchini Sudan.

Kamati Kuu ya Madaktari nchini humo imesema watu wawili waliuawa hapo jana kwa kufyatuliwa risasi katika mji mkuu Khartoum, huku wengine wawili wakiuawa katika mji wa Omdurman.

Tangazo hilo la uasi wa kiraia lililotolewa na Chama cha Wanataaluma wa Sudan SPA linakuja siku chache baada ya jeshi kuwashambulia waandamanaji na kusababisha makumi miongoni mwao kupoteza maisha mjini Khartoum na hivyo kuvunja matumaini ya makabidhiano ya kidemokasia ya madaraka.

Sehemu ya taarifa ya Chama cha Wanataaluma wa Sudan SPA imesema, "vuguvugu la uasi wa kiraia linaanza Jumapili na litaendelea hadi pale serikali ya kiraia itakapojitangaza yenyewe kupitia televisheni ya taifa."

Wanajeshi wa Sudan wakifanya msako mjini Khartoum

Haya yanajiri huku jeshi la Sudan likionekana kuanza kulegeza msimamo, licha ya hapo awali kukataa katakata kurejea katika meza ya mazungumzo na makundi ya wapinzani na waandamanaji.

Shamsuddin al Kabbashi, Msemaji wa Baraza la Kijeshi la Serikali ya Mpito ya Sudan ametangaza kuwa baraza hilo liko tayari kufanya mazungumzo bila ya masharti na Muungano wa Uhuru na Mabadiliko wa nchi hiyo, kwa lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo.

Hata hivyo Muungano wa Uhuru na Mabadiliko wa Sudan umesema kuwa ili kuendelea kufanya mazungumzo na Baraza la Kijeshi kuna udharura wa kuundwa kamati ya kimataifa ya kuchunguza mauaji ya makumi ya watu wakati askari usalama walipowavamia wapinzani waliokuwa katika mgomo wa kuketi chini mjini Khartoum.