Matangazo ya biashara yanayokiuka maadili marufuku Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5410-matangazo_ya_biashara_yanayokiuka_maadili_marufuku_kenya
Bodi ya Filamu nchini Kenya imepiga marufuku matangazo ya biashara yanayokiuka maadili mema katika redio, televisheni na maeneo ya umma nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 19, 2016 22:15 UTC
  • Matangazo ya biashara yanayokiuka maadili marufuku Kenya

Bodi ya Filamu nchini Kenya imepiga marufuku matangazo ya biashara yanayokiuka maadili mema katika redio, televisheni na maeneo ya umma nchini humo.

Akizungumza Jumanne na waandishi habari mjini Nairobi, mkuu wa bodi hiyo Ezekiel Mutua amesema matangazo yote ya biashara yanayosheheni lugha chafu, picha za ngono, matumizi ya pombe na kamari ni marufuku. Amesema bodi hiyo itahakikisha matangazo yote ya biashara hayakwendi kinyume na maadili ya kijamii au kuchochea ubaguzi wa kidini, kijinsi na kikabila. Hata hivyo bodi hiyo imesema marufuku hiyo katika vyombo vya habari itakuwa ikitekelezwa kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa nne usiku.

Aidha amesema matangazo ya biashara yenye kushajiisha maisha ya kianasa na kifakhari, uhusiano wa kingono wa watu wa jinsia moja, uasherati na utovu wa maadili utotoni ni marufuku kabisa nchini Kenya.

Mutua amesema taratibu hizo mpya zinalenga kulinda thamani na maadili ya taifa la Kenya na kuongeza kuwa matangazo ya biashara huwa na taathira kubwa kwa umma hasa watoto.

Halikadhalika amesema matangazo katika maeneo ya umma hasa mabango makubwa barabarani pia hayataruhusiwa kuwa na picha za watu walio uchi au nusu uchi kwani matangazo kama hayo huvuruga msingi wa familia.

Hivi karibuni kampuni ya Marekani ya vinywaji vya Coca Cola ililazimika kulifanyia mabadiliko tangazo lake la biashara ambalo lilipigwa marufuku na Bodi ya Filamu Kenya. Tangazo hilo lilikosolewa na umma kutokana na picha za kubusiana ambazo zlikiuka maadili ya kijamii nchini humo.