Muhammad Morsi aaga dunia mahakamani wakati kesi yake ikisikilizwa
(last modified Mon, 17 Jun 2019 20:03:31 GMT )
Jun 17, 2019 20:03 UTC
  • Muhammad Morsi aaga dunia mahakamani wakati  kesi yake ikisikilizwa

Muhammad Morsi rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia za kidemokrasia nchini Misri na kupinduliwa na jeshi ameaga dunia akiwa mahakamani kusikiliza kesi iliyokuwa ikimkabili.

Televisheni ya serikali ya Misri imetangaza kuwa Muhammad Morsi rais wa zamani wa nchi hiyo ameaga dunia leo Jumatatu kwa kiharusi akiwa mahakamani wakati kikao cha kusikiliza kesi yake kuhusu tuhuma zilizokuwa zikimkabili za kufanya ujasusi, kilipokuwa kikiendelea. 

Ripoti hiyo imeeleza kuwa, mwendazake Morsi alimuomba hakimu ampe fursa ya kuzungumza na hakimu akapewa. Baada ya kutangazwa kumalizika kikao hicho, ghafla Morsi alipoteza fahamu na kufariki dunia. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imetangaza hali ya hatari nchini humo kufuatia kifo cha rais  huyo wa zamani akiwa mikononi mwa vyombo vya dola.

Muhammad Morsi

Morsi aligombea  kiti cha urais mwaka 2012  akiiwakilisha harakati ya Ikhwanul Muslimin ya na aliibuka na ushindi katika kinyang'anyiro hicho dhidi ya Ahmad Shafiq, Waziri Mkuu wa mwisho wa aliyekuwa dikteta wa Misri Hosni Mubarak aliyeondolewa madarakani kwa mapinduzi ya wananchi.  

Morsi ambaye alikuwa Rais wa kwanza wa Misri asiye mwanajeshi,   Juni 3 mwaka 2013 yaani mwaka mmoja baada ya kuchaguliwa kuwa rais, alipinduliwa na kuondolewa madarakani kwa agizo la Abdel Fattah al Sisi kamanda wa jeshi la Misri. 

 

Tags