UN yataka Misri ifanye uchunguzi huru wa kifo cha Morsi
Ofisi ya Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa imesema ni matumaini yake kuwa uchunguzi huru na wa kina utafanyika juu ya mazingira ya kifo cha rais wa zamani wa Misri, Mohamed Morsi kilichotokea jana wakati akiwa mahakamani.
Msemaji wa ofisi hiyo, Rupert Colville amesema hayo kupitia taarifa iliyotolewa mjini Geneva Uswisi, baada ya ripoti kwamba siku ya Jumatatu Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri, alizimia wakati kesi yake ikiendelea mahakamani na hatimaye kuelezwa kuwa amefariki dunia.
Colville amesema kwa kuwa rais huyo wa zamani alikuwa korokoroni chini ya mamlaka za Misri wakati wa kifo chake, na serikali ilikuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa anatendewa utu na kwamba haki yake ya uhai na afya zinaheshimiwa.
Amesema kifo chochote cha ghafla wakati mtu yuko rumande kinapaswa kufuatiwa na uchunguzi wa haraka, wa kina na huru na ulio wazi ambao utafanywa na chombo kilicho huru ili kubainisha sababu za kifo.
Ofisi hiyo imetoa taarifa hiyo kufuatia wasiwasi ulioibuka juu ya mazingira aliyokumbana nayo Morsi wakati akiwa anashikiliwa, ukiwemo wa kukosa matibabu sahihi pamoja na kushindwa kukutana na mawakili na familia yake katika kipindi chote cha miaka 6 aliyokuwa korokoroni.
Mohammad Morsi ambaye aliondolewa madarakani kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na rais wa sasa, Abdulfattah al-Sisi tarehe 3 mwezi Julai mwaka 2013, alifariki dunia juzi wakati kesi iliyokuwa ikimkabili ikisikilizwa, na kuzikwa leo kimya kimya katika makaburi ya Medinat Nasr mashariki mwa Cairo, mji mkuu wa nchi hiyo.