Wakimbizi wa Ethiopia warejea katika nchi yao kutoka Yemen
Wakimbizi zaidi ya 2100 raia wa Ethiopia wamerejea nyumbani kutoka Yemen kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM.
Taarifa ya IOM iliyotolewa Ijumaa imesema ndege ya shirika hilo iliondoka jana Yemen kuelekea Ethiopia ikiwa na wahamiaji 96 hii ikiwa ni safari ya 18 kutoka Aden kwenda mjini Addis Ababa chini ya mpango wa kurejea nyumbani kwa khiari (VHR) tangu Mei 28 ukiwa umeshawasaidia jumla ya wahamiaji 2133 waliokuwa wamekwama Yemen wakiwemo watoto 750.
Tangu Aprili 21 mwaka huu mamlaka kwenye jimbo la Aden nchini Yemen ilianza kuwashikilia idadi kubwa ya wahamiaji wa kiholela na IOM inakadiria kwamba watu 5000 walikamatwa katika vituo vitatu vya wahamiaji.
Asilimia kubwa ya wahamiaji wanaorejea nyumbani kwa hiyari walikamatwa na wengi wao walishikiliwa kwa karibu miezi miwili katika vituo vinavyoshikilia wakimbizi mjini Aden.
Tangu Aprili IOM imekuwa ikiratibu hatua za kukabiliana na hali mbaya ya kibinadamu katika vituo hivyo ikitoa msaada wa dharura kama chakula, maji, usafi na huduma za afya kwa saa 24 kwa wahamiaji waliokuwa wanashukiliwa kwenye uwanja wa michezo.

Pia imeanzisha kituo cha kutibu magonjwa ya kuhara (DTC) katika hospitali ya Ibn Khaldoon kuwasaidia wahamiaji wanaokabiliwa na magonjwa ya kuharisha.
Hadi sasa IOM imeshasaidia wahamiaji 2000 kurejea nyumbani kwa usalama na wengine 2000 bado wako kwenye kiwanja cha michezo wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto na katika wiki zijazo IOM itawasaidia watoto waliobaki kurejea nyumbani kwa hiyari.
Shirika la IOM linasema licha ya vita vinavyoendelea Yemen wahamiaji wanaokwenda kusaka fursa katika nchi za Ghuba ya Uajemi wanaendelea kufanya safari za hatari kupitia, nchi kavu na bahari na njia nzima wahamiaji hao hukumbana na changamoto nyingi za kupata ulinzi na msaada.