Wapinzani Ethiopia watahadharisha kuhusu kuahirishwa uchaguzi wa 2020
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54274-wapinzani_ethiopia_watahadharisha_kuhusu_kuahirishwa_uchaguzi_wa_2020
Wanasiasa wa mrengo wa upinzani nchini Ethiopia wametahadharisha kuhusu uwezekano wa kuahirishwa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwaka 2020 ambao unatazamiwa kuwa wa kwanza chini ya waziri mkuu mpenda mageuzi Abiy Ahmad. Wamesema yamkini uchaguzi ukaahirishwa kutokana na uhasama wa kikabila unaoendelea kutokota katika maeneo mbali mbali nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 22, 2019 02:58 UTC
  • Wapinzani Ethiopia watahadharisha kuhusu kuahirishwa uchaguzi wa 2020

Wanasiasa wa mrengo wa upinzani nchini Ethiopia wametahadharisha kuhusu uwezekano wa kuahirishwa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwaka 2020 ambao unatazamiwa kuwa wa kwanza chini ya waziri mkuu mpenda mageuzi Abiy Ahmad. Wamesema yamkini uchaguzi ukaahirishwa kutokana na uhasama wa kikabila unaoendelea kutokota katika maeneo mbali mbali nchini humo.

Mapema mwezi huu, tume ya uchaguzi Ethiopia ilitangaza kuwa zaidi ya watu milioni 2.4 wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na ukosefu wa usalama.

Tayari sensa ya kitaifa imeshaahirishwa mara mbili jambo ambalo yamkini likaathiri vibaya maandalizi ya uchaguzi na uchorwaji wa mipaka mipya ya maeneo bunge.

Wapinzani wanasema kuahirishwa uchaguzi wa kitaifa kunaweza kusababisha matatizo makubwa na kuchochea zaidi malumbano baina ya maeneo kadhaa nchini humo na hivyo kutia dosari mchakato wa mabadiliko ya kidemokrasia ambayo Abiy ameyaanzisha.

Akizungumza na shirika la habari la Reuters, mfungwa wa zamani wa kisiasa Merera Gudina amesema iwapo serikali itaahirisha uchaguzi mkuu, basi hatua hiyo itaibua hasira kubwa katika jamii. Gudina ni mwanachama wa chama cha upinzani cha Oromo Federalist Congress kutoka eneo la Oromia ambalo limekuwa kitovu cha maandamano dhidi ya serikali katika miaka ya hivi karibuni.

Naye Belete Mola, naibu mkuu wa Harakati ya Kitaifa ya Amhara ambayo inawakilisha kabila la Amhara ametahadharisha kuwa serikali inachezea moto kwa kupanga kuahirisha uchaguzi. Kwa upande wake, Debretsion Gebremichael wa chama cha Tigray People’s Liberation Front (TPLF) ambaye pia ni makamu wa rais wa eneo la Tigray ametahadharisha kuhusu mgogoro utakaoibuka iwapo uchaguzi utaahirishwa. Chama cha TPLF kiko katika muungano tawala.

Wananchi takribani milioni 100 nchini Ethiopia wameanza kushuhudia mabadiliko makubwa ya kisiasa. Abiy Ahmed ambaye alichukua madaraka mwaka jana amewaachilia huru waandishi habari na wanaharakati wa kisiasa na kuondoa marufuku ya vyama vya kisiasa sambamba na kuwafikisha kizimbani maafisa wa serikali wanaotuhumiwa kukiuka haki za binadamu.

Mapema mwezi huu mkuu wa tume ya uchaguzi Ethiopia Birtukan Mideksa alikiri kuwa bado wako nyuma katika matayarisho ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Mei mwaka 2020.