Mkuu wa Jeshi la Ethiopia auawa katika jaribio la mapinduzi
Mkuu wa Jeshi la Ethiopia Jenerali Seare Mekonnen na maafisa wengine watatu wa ngazi za juu wameuawa katika jaribio la kuipindua serikali ya jimbo la Amhara kaskazini mwa nchi hiyo.
Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni akiwa amevalia sare za kijeshi , Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amethibitisha kuuawa mkuu wa jeshi la nchi hiyo. Taarifa zinasema Rais wa Jimbo la Amhara, Ambachew Mekonnen na mshauri wake pia wameuawa katika jaribio hilo la mapinduzi ambalo lilitekelezwa na mkuu wa usalama katika eneo hilo Jenerali Asamnew Tsige.
Serikali ya Abiy Ahmed inakabiliwa na mashinikizo kutoka kwa baadhi ya watu wenye ushawishi mkubwa katika majimbo ya nchi hiyo, likiwemo jimbo la Amhara, ambalo limekuwa kitovu cha mapigano ya kikabila nchini Ethiopia. Mfumo wa utawala wa Ethiopia ni wa kifederali au majimbo na kila jimbo lina rais mwenye mamlaka ya ndani.
Ufyatuaji risasi huko Amhara umejiri wakati maafisa wa jimbo walipokuwa wakikutana na rais wa jimbo hilo ambaye ni muitifaki wa Abiy. Walikuwa wamekutana kujadili njia ya kumzuia Jenerali Asamnew kusajili wapiganaji wa kikabila.

Wiki iliyopita Jenerali Asamnew aliwatangazia wazi watu wa kabila la Amhara, moja ya makabila makubwa Ethiopia, kujizatiti kwa silaha hatua ambayo imeeneza wasiwasi katika nchi hiyo.
Wananchi takribani milioni 100 nchini Ethiopia wameanza kushuhudia mabadiliko makubwa ya kisiasa. Abiy Ahmed ambaye alichukua madaraka mwaka jana amewaachilia huru waandishi habari na wanaharakati wa kisiasa na kuondoa marufuku ya vyama vya kisiasa sambamba na kuwafikisha kizimbani maafisa wa serikali wanaotuhumiwa kukiuka haki za binadamu.