Mwana wa Morsi ahadithia alivyopewa maiti ya baba yake, asisitiza ameuawa
Abdullah Morsi mwana wa kiume wa aliyekuwa rais wa Misri Muhammad Morsi aliyefariki dunia siku chache zilizopita akiwa kizimbani kusikiliza kesi iliyokuwa ikimkabili amehadithia jinsi alivyokabidhiwa mwili wa baba yake na jinsi alivyoaga dunia.
Abdullah Morsi amesema kuwa utawala wa Misri umefanya jinai ya mauaji ya polepole dhidi ya rais wa zamani wa nchi hiyo ili kutaka kuonesha kuwa amekufa kifo cha kawaida.
Amesema kuwa vyombo vya usalama vya Misri vilimtaka atie saini hati ya kupokea mwili wa baba yake kabla hata ya kupewa maiti hiyo na akiri kuwa kifo chake kilikuwa cha kawaida. Amesema mazingira yaliyoandamana na kukabidhiwa maiti ya Muhammad Morsi na kuiosha yalikuwa ya kudhalilisha. Abdullah Morsi amesema kuwa serikali ya Cairo imemzuia kuzungumzia mazingira ya kifo cha baba yake lakini familia yake inasisitiza kuwa haitanyamaza kimya na kwamba imepokea vitisho vingi kutoka kwa serikali ya Misri.
Amesisitiza kuwa jaribio la kutaka kumuua baba yake lilianza tangu miaka 6 iliyopita na kwamba familia yake iliripoti suala hilo katika kipindi chote hjicho. Mwana wa kiume wa Muhammad Morsi ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusu sababu halisi ya kifo chake na kusema Morsi alikuwa akinyanyaswa mara kwa mara kwa mpangilio maalumu.
Abdullah Morsi amewataka Wamisri kushikamana kwa ajili ya kukabiliana na utawala wa Misri ambao amesema unatenda jinai na umehusika na mauaji ya wanajeshi na polisi katika eneo la Sinai.
Siku kadhaa zilizopita pia Abdullah Morsi aliandika katika mtandao wa kijamii wa Twetter kwamba Rais Abdel Fattah al Sisi na maafisa wa serikali yake ndio waliomuua baba yake, Mohammad Morsi.
Rais huyo za zamani wa Misri Jumatatu iliyopita alianguka chini na kupoteza fahami na kisha akaaga dunia alipokuwa mahakamani kusikiliza kesi yake. Baada tu ya kifo hicho, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri ilitangaza hali ya hatari kote nchini humo.
Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imeripoti kuwa, katika kikao cha kusikiliza kesi yake kilichofanyika tarehe 7 Mei, Muhammad Morsi alisema kuwa maisha yake yalikuwa hatarini. Al Jazeera imeongeza kuwa, rais huyo wa zamani wa Misri aliyepinduliwa na jeshi mwaka 2013 alipitisha karibu nusu saa tangu alipoanguka na kuzimia mahakamani bila ya kuchukuliwa hatua yoyote ya maana ya kumpa huduma ya awali au matibabu.