Jun 25, 2019 13:00 UTC
  • Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lakutana Morocco

Mkutano wa 12 wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika unaendelea mjini Skhirat nchini Morocco.

Mkutano huo wa siku tatu ambao ulianza Jumatatu unajadili njia za kuleta amani katika bara la Afrika ambalo hivi sasa linashuhudia misukosuko ya kisiasa na ukosefu wa usalama katika nchi kadhaa.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo, waziri wa Morocco anayeshughulikia ushirikiano wa Afrika, Mohcine Jazouli, amesema mageuzi ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika yanatakiwa kufuata vigezo vya kimsingi vinavyoweza kuleta mabadiliko halisi.

Ameongeza kuwa Morocco inalialika baraza hilo kuimarisha hatua zake chini ya ushirikiano na tume ya kujenga amani ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kutimiza amani ya kudumu barani Afrika.

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Morocco, mkutano huo wa siku tatu unaofanyika kabla ya Morocco kuwa mwenyekiti wa zamu wa baraza hilo, utatathmini hatua za kujenga amani barani Afrika, mfumo wa utendaji kazi wa baraza hilo, pamoja na changamoto zinazokabili usimamizi na utatuzi wa migogoro barani humo.

Mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika unaofanyika nchini Morocco

Mwaka 2017, Umoja wa Afrika AU ulikubali tena uanachama wa Morocco baada ya miaka 33 wakati nchi hiyo ilijiondoa katika umoja huo kutokana na mgogoro wa Sahara Magharibi ambao hadi sasa haujatatuliwa. Hata hivyo Afrika Kusini na Algeria ni miongoni mwa nchi ambazo zilipinga Morocco kurejea katika AU.

Mwaka 1984 Morocco ilijiondoa katika Umoja wa Afrika AU, wakati huo ukijulikana kama OAU, baada ya eneo la Sahara Magharibi kukubaliwa kama mwanachama wa umoja huo.

Morocco ilichukua udhibiti wa Sahara Magharibi kutoka mkoloni Mhispania mwaka 1975  na inasisitiza kuwa eneo hilo ni sehemu ya ardhi yake. Hata hivyo aghalabu ya nchi duniani zinapinga hatua hiyo ya Morocco.

 

Tags