Mjumbe mpya wa UN Somalia apongeza vikosi vya AMISOM
Mjumbe mpya wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia James Swan amepongeza mchango uliotolewa na vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) kutokana na juhudi zinazoendelea kuituliza Somalia.
Swan ameahidi kushirikiana na AMISOM kusaidia kuunga mkono juhudi za amani nchini Somalia huku akisisitiza kuwa Umoja wa Afrika ni mshirika muhimu wa Umoja wa Mataifa.
Swan aliteuliwa mwezi Mei na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres na tayari ameshakutana na maofisa waandamizi wa AMISOM wakiongozwa na mwakilishi maalumu wa kamati ya Umoja wa Afrika Fracisco Madeira kwenye kazi yake ya kwanza nchini Somalia.
Umoja wa Mataifa unafadhili askari hao wa Amisom ambao sasa ni 21,000 na wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007. Wanajeshi wa Amisom walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone. Nao maafisa wa polisi wa AMISOM ni kutoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda.
Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 na katika miaka ya hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wakufurishaji wa Al Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.