Baraza la Usalama laongeza muda wa vikwazo dhidi ya Kongo DR
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeongeza muda wa vikwazo dhidi ya shakhsia kadhaa wakiwemo makamanda wa jeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa mwaka mmoja zaidi.
Vikwazo hivyo ni pamoja na vya silaha, kusafiri na kuzuia mali za shakhsia hao hadi mwezi Julai mwakani. Azimio hilo nambari 2478 limepasishwa kwa kishindo, kwani limeungwa mkono na wajumbe 15 wa baraza hilo.
Baraza la Usalama pia limeongeza muda kuendelea kuhudumu wataalamu wa Kamati ya Vikwazo hadi Agosti Mosi mwaka ujao 2020.
Azimio hilo limewataka wataalamu hao kuwasilisha ripoti yake ya mwisho kabla ya Juni 15, 2020 kwa Kamati ya Vikwazo ya Baraza la Usalama la UN.
Baraza la Usalama limepasisha azimio hilo siku chache baada ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR kusema zaidi ya watu laki tatu wameikimbia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita, kutokana na mapigano ya kikabila.
Kadhalika maafisa wa serikali ya DRC walisema watu 161 waliuawa hivi karibuni kutokana na mapigano mapya baina ya jamii za wafugaji na wakulima katika mkoa huo.