Wanigeria waandamana kupinga kundi linalodai kuwa eti linapambana na Boko Haram
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54487-wanigeria_waandamana_kupinga_kundi_linalodai_kuwa_eti_linapambana_na_boko_haram
Kufutia mauaji ya dereva mmoja kaskazini mashariki mwa Nigeria yaliyofanywa na kundi la wanamgambo linalodai kuwa linapambana na wanamgambo wa Boko Haram, maelfu ya Wanigeria wamefanya maandamano makubwa wakitaka kuhitimishwa shughuli za kundi hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 01, 2019 08:22 UTC
  • Wanigeria waandamana kupinga kundi linalodai kuwa eti linapambana na Boko Haram

Kufutia mauaji ya dereva mmoja kaskazini mashariki mwa Nigeria yaliyofanywa na kundi la wanamgambo linalodai kuwa linapambana na wanamgambo wa Boko Haram, maelfu ya Wanigeria wamefanya maandamano makubwa wakitaka kuhitimishwa shughuli za kundi hilo.

Zaidi ya watu 2000 katika mji wa Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo wameshiriki maandamano hayo makubwa ya kupinga kundi hilo. Waandamanaji hao walifunga barabara kuu ya mji wa Maiduguri na wametangaza kwamba kundi hilo linatumia vibaya mapambano yake dhidi kundi la Boko Haram na kwa msingi huo wametaka kukomeshwa haraka shughuli zake katika mji huo.

Kundi la Boko Haram, wenzo wa kuibuka makundi ya kihalifu nchini Nigeria

Maandamano hayo yalifanyika masaa machache baada ya wanachama wa kundi hilo kumshambulia na kumpiga risasi dereva mmoja katika kituo cha upekuzi na kumuua.

Jimbo la Borno limekuwa likishuhudia mashambulizi ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram tangu mwaka 2009. Hujuma hizo zilivuka mipaka hadi katika nchi jirani ambapo zaidi ya watu elfu 20 wameuawa hadi sasa na wengine zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi.