Maandamano makubwa Sudan; sisitizo la kufanyika harakati katika mkondo wa demokrasia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54509-maandamano_makubwa_sudan_sisitizo_la_kufanyika_harakati_katika_mkondo_wa_demokrasia
Jumapili ya juzi nchi ya Sudan ilishuhudia moja ya siku ngumu zaidi tangu Omar Hassan al-Bashir Rais wa zamani wa nchi hiyo aondolewe madarakani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 02, 2019 08:26 UTC
  • Maandamano makubwa Sudan; sisitizo la kufanyika harakati katika mkondo wa demokrasia

Jumapili ya juzi nchi ya Sudan ilishuhudia moja ya siku ngumu zaidi tangu Omar Hassan al-Bashir Rais wa zamani wa nchi hiyo aondolewe madarakani.

Wapinzani nchini Sudan walimiminika katika mitaa na barabara za miji mbalimbali ya nchi hiyo kwa wito wa Muungano wa Uhuru na Mageuzi ambacho ni chama kikubwa zaidi kinacholipinga Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan. Hata hivyo maandamano hayo yaliyofanyika kwa lengo la kulalamikia na kupinga kigugumizi cha Baraza la Kijeshi la Mpito cha kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia yalikabiliwa na mkono wa chuma na ukandamizaji mkubwa ambapo kwa akali watu 7 waliuawa na wengine zaidi ya 180 walijeruhiwa. 

Kwa hakika hali ya mambo nchini Sudan ni ya mgogoro na mazungumzo baina ya muungano wa upinzani na majenerali wa jeshi yamekwama baada ya ukandamizaji wa vikosi vya usalama wa tarehe 3 ya mwezi uliopita wa Juni ambapo raia 118 waliuawa. Waandamanaji nchini Sudan  wanasisitiza kuwa, wataendeleza uasi wa kiraia hadi pale watakapofikia malengo yao. Waandamanaji hao mbali na kusisitiza kuuendeleza maandamano ya amani wanasema kuwa, hawawezi kuvumilia kigugumizi na chelewa chelewa ya Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan ya kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.  Lililo wazi ni kuwa, takwa kuu la wananchi hao ni kukabidhiwa madaraka kwa utawala wa kiraia na hivyo kuiweka nchi hiyo katika mkondo wa kuundwa serikali ya kidemokrasia kwa kufanyika uchaguzi huru.

Majenerali wa Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan

Ali Mahjoub mmoja wa maafisa wa Chama cha Kikomonisti cha Sudan anasema kuwa: Tunalitaka Baraza la Kijeshi la Sudan likabidhi madaraka ya nchi kwa serikali ya kiraia ambayo inataka kuweko demokrasia kamili katika nchi. Watu ambao wanashiriki katika maandamano ni raia ambao wanataka amani; lakini inasikitisha kuona kwamba, Baraza la Kijeshi hakuna linachokitambua ghairi ya mabavu na ukandamizaji.

Aidha waandamanaji nchini Sudan wanawaona baadhi ya wajumbe katika timu ya majerali wa kijeshi wanaoongoza nchini humo kwamba, ni watu vibaraka ambao wanatekeleza amri na maagizo ya madola ya kigeni hususan Saudi Arabia, Misri na Imarati. Kwa mtazamo wa wananchi hao ni kuwa, mauaji ya Juni 3 mwaka huu nayo yalifanyika kwa idhini na kwa baraka za Saudi Arabia, Imarati na Misri. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana moja ya matakwa ya wananchi wa Sudan ni kukomeshwa uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi yao.

Siddiq Abu Fawaz, mmoja wa wapinzani wa Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan amefichua kuhusu himaya na uungaji mkono mkubwa wa Saudi Arabia na Imarati kwa majenerali wa kijeshi wanaotawala nchini Sudan pamoja na vifurushi vinavyopakuliwa na ndege za Saudi Arabia katika Uwanja wa Ndege wa Khartoum  na kusema kuwa, inaonekana vifurushi na mizigo hiyo ya Saudi Arabia na Imarati iliyopakuliwa katika Uwanja wa Ndege wa Khartoum katika majuma ya hivi karibuni ni zana za kijeshi na kivita.

Maandamano ya wananchi wa Sudan

Maandamano ya Jumapili iliyopita ya wananchi wa Sudan ni ya pili makubwa baada ya yale ya Juni 3 ambayo haya nayo kama yalivyokuwa yale yaliyopita yalikabiliwa na ukandamizaji na umwagaji damu mkubwa wa vikosi vya usalama. 

Licha ya kuwa viongozi wa upinzani na majenerali wa kijeshi  wameacha kukutana katika meza ya mazungumzo, lakini kungali kunafanyika juhudi za mpatishi wa mgogoro huo yaani Ethiopia pamoja na mashinikizo ya jamii ya kimataifa yenye lengo la kuupatia ufumbuzi mzozo huo kwa njia ya mazungumzo. Baada ya kushika kasi azma na irada ya wapinzani ya kuendelea na uasi wa kiraia,  viongozi wa Baraza la Kijeshi wametangaza tena utayari wao wa kuanza mazungumzo na kusisitiza kwamba, utatuzi wowote wa mgogoro huo unapaswa kufanyika chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika. Kwa mtazamo wa majerali hao ni kuwa, mpango wa Ethiopia unaweza kuwa  jiwe zuri la msingi kwa ajili ya kuanza mazungumzo.

Hata hivyo Muungano wa Uhuru na Mageuzi unataka kuundwe Kamati ya Kimataifa ya Kutafuta Ukweli kuhusiana na mauaji ya Juni 3 mjini Khartoum, kuachiliwa huru wafungwa wote wa kisiasa, kurejeshwa mawasiiliano ya Intaneti na majerali wa kijeshi kuomba radhi rasmi kutokana na ukandamizaji na mauaji dhidi ya wapinzani katika miezi ya hivi karibuni.

Wapinzani nchini Sudan ambao katika miezi iliyopita walishindwa kuvumilia sera za Omar al-Bashir, hawajasalimu amri mbele ya mazingira yaliyojitokeza baada ya kupinduliwa al-Bashir, na filihali wangali wanafanya juhudi kwa nguvu zao zote ili kuhakikisha kwamba, nchi hiyo inashuhudia mageuzi na mabadiliko ya kimsingi na hivyo kuifanya nchi yao ielekee kwenye mkondo wa demokrasia.