Somalia yakata uhusiano na Guinea, yaituhumu Conakry kuingilia masuala yake ya ndani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54574-somalia_yakata_uhusiano_na_guinea_yaituhumu_conakry_kuingilia_masuala_yake_ya_ndani
Serikali ya Somalia imekata uhusiano wake wote wa kidiplomasia na Guinea Conakry na kuituhumu nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kuwa inaingilia masuala yake ya ndani.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jul 05, 2019 10:44 UTC
  • Somalia yakata uhusiano na Guinea, yaituhumu Conakry kuingilia masuala yake ya ndani

Serikali ya Somalia imekata uhusiano wake wote wa kidiplomasia na Guinea Conakry na kuituhumu nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kuwa inaingilia masuala yake ya ndani.

Wakati serikali ya Somalia ikikata uhusiano wake wote na nchi hiyo na kuituhumu Conakry kuwa inaingilia masuala ya ndani ya Somalia imesema pia kuwa Guinea Conakry inahatarisha umoja wa ardhi ya nchi hiyo. 

Ahmed Isse Awad, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Somalia amesema wakati anatangaza habari hiyo kwamba, serikali ya Conakry imempokea kwa heshima zote za rais wa nchi, Muse Bihi Abdi, aliyejitangaza kuwa rais wa Somaliland kinyume cha sheria. Serikali ya Mogadishu inasema kuwa, huo ni uvunjaji wa wazi wa maazimio ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.

Mji wa Hargeisa, Somaliland, Somalia

 

Eneo la Somaliland lililojitangazia uhuru wake linaundwa na mikoa mitano ya kaskazini mwa Somalia. Lilitangaza kujitenga na Somalia mwaka 1991 na kuitangaza Hargeisa kuwa mji wake mkuu. Hata hivyo hadi hivi sasa hakuna nchi yoyote duniani inayoitambua Somaliland kuwa ni nchi huru.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia amezionya nchi nyingine zenye muelekeo wa kutaka kuitambua rasmi Somaliland kuwa nchi huru na kusema kuwa, serikali ya Mogadishu haiwezi kufumbia macho hata shibri moja ya ardhi ya Somalia.