Mogadishu yatahadharisha kuhusu kuingiliwa masuala ya ndani ya Somalia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia ametahadharisha kuhusu uingiliaji wa baadhi ya nchi katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na kukitaja kitendo hicho kuwa ni kukiuka mamlaka ya kujitawala nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Ahmad Isse Awad aliyezungumza jana Jumamosi amewatolea wito walimwengu wazuie uingilijiai huo wa baadhi ya nchi katika masuala ya ndani ya Somalia. Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia ameongeza kuwa ujumbe huu unapasa kuzifikia nchi husika kwamba Somalia kamwe haitaafiki kuanzishwa uhusiano na upande wowote wa Kisomali bila ya serikali kuu kuwa na taarifa. Ahmad Isse Awad ameyasema hayo huko Mogadishu mji mkuu wa nchi hiyo baada ya mazungumzo kati yake na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao huko Somalia. Amesema Mogadishu inajua ni kwa namna gani itatatua matatizo yake ya ndani, lakini kwamba jambo hili litawezekana tu pale baadhi ya nchi zitakapoacha kuzusha migawanyiko kati ya Wasomali.
Serikali ya Somalia siku mbili zilizopita iliashiria namna Jamhuri ya Guinea Conakry ilivyoanzisha uhusiano wa karibu na eneo la Somaliland lililojitangazia uhuru wake, jambo lililopelekea uchukue uamuzi wa kakata uhusiano wake wa kidiplomasia na nchi hiyo.
Eneo la Somaliland lililojitangazia uhuru wake linaundwa na mikoa mitano ya kaskazini mwa Somalia. Lilitangaza kujitenga na Somalia mwaka 1991 na kuitangaza Hargeisa kuwa mji wake mkuu. Hata hivyo hadi sasa hakuna nchi yoyote duniani inayoitambua rasmi Somaliland kuwa ni nchi huru.