Misri kuwauzia wageni uraia wa nchi hiyo kwa dola elfu kumi
(last modified Mon, 08 Jul 2019 11:27:16 GMT )
Jul 08, 2019 11:27 UTC
  • Misri kuwauzia wageni uraia wa nchi hiyo kwa dola elfu kumi

Bunge la Misri limekubaliana na mpango wa serikali ya nchi hiyo kwa kuwauzia uraia wageni kwa dola elfu kumi za Kimarekani licha ya baadhi ya wabunge kupinga suala hilo.

Televisheni ya Sky News imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Bunge la Misri limekubaliana na sheria ya kutoa kibali cha kuishi na uraia kwa wageni wanaongia nchini humo na limeirejesha sheria hiyo kwa serikali ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa. 

Muswada wa sheria hiyo ulipasishwa jana (Jumapili) na Bunge la Misri na unahusiana na kuingia raia wa kigeni nchini Misri na kuwa na haki ya kuishi. Sheria hiyo inairuhusu pia serikali ya Misri kuuza uraia wa nchi hiyo kwa raia wa kigeni.

Baadhi ya wabunge wa Misri wametia saini kwenye tambara kubwa kupinga jambo hilo na kusema kuwa njama hizo zina uhusiano wa moja kwa moja na mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne.

Cairo, mji mkuu wa Misri

 

Hata hivyo spika wa Bunge la Misri, Ali Abdel Aal amedai kuwa uamuzi huo umefikiwa kwa sababu tu ya kuvutia wawekezaji wa kigeni.

Kwa mujibu wa mpango wa kiuadui wa Marekani wa Muamala wa Karne, mji wa Baytul Muqaddas wenye Msikiti wa al Aqsa ambacho ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu watapewa Wazayuni, wakimbizi wa Palestina wanaoishi nje hawatokuwa na haki ya kurudi kwao, bali watamegewa vipande vya ardhi katika baadhi ya nchi za Kiarabu na wale walioko katika ardhi za Palestina watakuwa wanamiliki baadhi ya vipande vya ardhi tu vya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza. Mpango huo umepingwa vikali na makundi yote ya Palestina.

Tags