Jul 15, 2019 10:24 UTC
  • Mkutano wa Baraza la Kijeshi la Sudan na kambi ya upinzani waakhirishwa

Muungano wa Uhuru na Mabadiliko nchini Sudan umetangaza kuwa, mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika leo na wawakilishi wa Baraza la Kijeshi linalotawala nchi hiyo chini ya upatanishi wa Ethiopia na Umoja wa Afrika umeakhirishwa hadi Jumanne ya kesho.

Afisa mmoja wa muungano huo amesema, mkutano huo umeakhirishwa ili kushauriana zaidi juu ya waraka wa makubaliano ya kugawana madaraka na sheria za kipindi cha mpito.

Jumamosi iliyopita Muungano wa Uhuru na Mabadiliko ulikuwa umetangaza kuwa, hauafikiani na baadhi ya vipengee vilivyowekwa kwenye waraka huo na kwamba vinapaswa kuajadiliwa zaidi.

Habari zinasema kuwa, waraka huo uliotayarishwa kwa ajili ya kipindi cha mpito cha miaka mitatu nchini Sudan umepuuza masuala mengi muhimu ikiwa ni pamoja na kadhia ya amani na wakimbizi. Ripoti zinasema suala jingine lililozusha hitilafu baina ya pande hizo mbili ni kinga kamili ya kutofikishwa mahakamani inayotolewa kwa mwenyekiti na wajumbe wa baraza la uongozi katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya mpito.

Mkutano wa amani Sudan waakhirishwa

Awali mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mgogoro wa Sudan, Mohammed Hassan Labat alikuwa amesema pande mbili hasimu zimefikia makubaliano kamili juu ya waraka wa kisiasa unaoainisha taasisi na majukumu yote ya kipindi cha mpito.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, kipindi cha mpito kitakuwa cha miaka mitatu na miezi mitatu na baraza litakaloongoza nchi hiyo litakuwa na wajumbe watano wanajeshi na wajumbe watano raia. Uwenyekiti wa baraza hilo utakuwa wa kupokezana.

Baraza la Kijeshi la Sudan lilitwaa madaraka Aprili mwaka huu baada ya kumpindua Omar al-Bashir aliyeiongoza nchi hiyo kwa karibu miongo mitatu, kufuatia wimbi la maandamano ya wananchi.

 

Tags