Watu 17 wauawa katika mripuko wa bomu Somalia, Al Shabaab latangaza kuhusika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54941-watu_17_wauawa_katika_mripuko_wa_bomu_somalia_al_shabaab_latangaza_kuhusika
Watu wasiopungua 17 wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa nchini Somalia wakati bomu liliporipuka nje ya hoteli moja karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa ulioko kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 23, 2019 03:06 UTC
  • Watu 17 wauawa katika mripuko wa bomu Somalia, Al Shabaab latangaza kuhusika

Watu wasiopungua 17 wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa nchini Somalia wakati bomu liliporipuka nje ya hoteli moja karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa ulioko kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.

Afisa wa polisi Ahmed Bashane amevieleza vyombo vya habari kuwa mshambuliaji wa kujitoa mhanga aliligongesha gari lenye mada za miripuko na kituo cha upekuzi kilichoko kwenye barabara kuu inayoelekea uwanja wa ndege.

Ameongeza kuwa, wamekusanya maiti na kuthibitisha vifo vya watu 17 akiwemo gaidi aliyefanya shambulio hilo.

Kundi la kigaidi la Al Shabaab limetangaza kuhusika na shambulio hilo ambalo lilitokea jana kwenye kituo hicho cha upekuzi kilichoko nje ya hoteli ya Afrik.

Wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al Shabaab

Nura Hassan, muuguzi katika hospitali ya Madina iliyoko mjini Mogadishu amesema, hospitali hiyo imepokea watu 27 waliojeruhiwa, 17 kati yao wakiwa na majeraha makubwa.

Shambulio hilo la jana limetokea baada ya kupita takriban wiki moja tangu watu 26 walipouawa na wengine 56 walipojeruhiwa katika shambulio lililoendelea kwa muda wa saa 12 lililofanywa na magaidi wa kundi la Al Shabaab katika hoteli moja maarufu iliyoko kwenye mji wa bandari wa Kismayo kusini mwa Somalia.../