Juhudi za Waislamu wa Nigeria na kuachiliwa kwa masharti Sheikh Ibrahim Zakzaky
Baada ya kupita mwezi mmoja tangu kutangazwa habari ya kuzidi kuzorota hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria na juhudi za Waislamu wa nchi hiyo za kutaka kuachiliwa huru mwanaharakati huyo, hatimaye Jumatatu ya juzi tarehe 6 Agosti, Mahakama Kuu ya Kaduna ilitoa hukumu ya kuachiwa huru mwanaharakati huyo ili asafiri kuelekea nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Mara baada ya kuachiliwa huru, Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe wanatarajiwa kusafiri kuelekea nchini India kwa ajili ya matibabu. Hata hivyo safari ya Sheikh Zakzaky kuelekea India itafanyika kwa masharti maalumu, likiwemo la kuandamana maafisa wa usalama wa Nigeria na kiongozi huyo wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo katika safari yake hiyo.
Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe walitiwa nguvuni na askari wa jeshi la Nigeria Desemba 13, 2015 katika shambulio na uvamizi uliofanywa na askari hao dhidi ya Huseiniya ya mji wa Zaria nchini humo.
Siku waliyomtia nguvuni Sheikh Zakzaky, askari wa jeshi la Nigeria waliwafyatulia risasi watu waliokuwa wamejumuika kwenye Hussainiya hiyo na mbele ya nyumba ya kiongozi huyo wa kidini na kuwaua shahidi mamia miongoni mwao wakiwemo watoto wake watatu wa kiume.
Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa amri ya kuachiliwa huru mara moja mwanachuoni huyo mwezi Disemba 2016 na kuliwajibisha jeshi la nchi hiyo kulipa fidia ya dola laki moja na 50 elfu kwa familia ya Sheikh Zakzaky. Hata hivyo jeshi, serikali na vyombo vya dola vya Nigeria vilikataa kutekeleza amri hiyo ya mahakama na kuendelea kumweka korokoroni mwanchuoni huyo kinyume cha sheria.
Licha ya kuwa, tangu Sheikh Ibrahim Zakzaky atiwe mbaroni, Waislamu wa Nigeria wamekuwa wakifanya mikusanyiko na maandamano wakitaka kuachiliwa huru mwanazuoni huyo, lakini baada ya kutangazwa habari ya kuzidi kuzorota afya ya Sheikh Zakzaky, maandamano ya Waislamu hao pamoja na mikusanyiko ilishadidi.
Hata hivyo maandamano na mikusanyiko hiyo ilikabiliwa na mkono wa chuma wa vikosi vya usalama vya Nigeria sambamba na kimya cha jumuiya na asasi za kimataifa kinachoongeza. Fauka ya hayo, ofisi ya Rais Muhamadu Buhari ikachukua hatua ya kuitangaza Harakati ya Kiislamu ya Nigeria kuwa kundi la kigaidi na ikapiga marufuku shughuli za harakati hiyo.
Mmoja wa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Bayero nchini Nigeria anasema: Mawahabi ndiyo chimbuko kuu la mashinikizo dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo. Viongozi wa Nigeria wamekuwa wakipatiwa fedha na watawala wa Saudi Arabia na kutokana na umasikini wako tayari kufanya chochote. Baadhi ya makamanda wa jeshi la polisi na hata mawaziri, wamekuwa wakipatiwa fedha na Saudia. Watawala wa Saudia wameitaka serikali ya Nigeria izuie kasi ya kuenea madhehebu ya Shia katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Waislamu wa Nigeria si tu kwamba, hawaridhishwi na utendaji wa serikali ya Abuja katika uwanja huo, bali wanalalamikia pia kimya cha asasi na jumuiya za kimataifa mkabala na utendaji wa serikali ya Abuja na ukiukaji wake wa haki za binadamu dhidi ya Sheikh Zakzaky. Waungaji mkono wa Sheikh Ibrahim Zakzaky wanaamini kwamba, suala la haki za binadamu ni kadhia ya kimataifa na hilo linapaswa kuzingatiwa pia kwa Sheikh Zakzaky. Hata hivyo viongozi na maafisa usalama wa Nigeria wamepuuza hilo.
Katika uwanja huo, hivi karibuni wasomi na wanafikra mashuhuri 52 wa vyuo vikuu walimuandikkia barua Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakimtaka asaidie jitihada za kutaka kuachiwa huru mara moja Sheikh Ibrahim Zakzaky huko Nigeria kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Hivi sasa inaonekkana kuwa, serikali ya Nigeria imelazimika kumuachia huru kwa masharti Sheikh Zakzaky baada ya kushadidi mashinikizo dhidi yake na kumruhusu akatibiwe nchini India. Hata kama hukumu hiyo ya mahakkama inaweza kuhesabiwa kuwa ni ushindi kwa Waislamu wa Nigeria na kuzaa matunda juhudi zao, lakini bado kuna safari ndefu hadi kutekelezwa kivitendo hukumu hiyo.
Sheikh Abdalla Zengo, mmoja wa wanafunzi wa masomo ya dini na mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Nigeria anasema kuhusiana na suala hilo kwamba, Sheikh Zakzaky amewaamsha wananchi na kuwaambia Waislamu kwamba, kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'ani hawapaswi kudhulumu wala kuikubali dhulma. Misimamo na mitazamo ya Sheikh Zakzaky inahesabiwa kuwa tishio kubwa kwa wanasiasa wa Nigeria.