Aug 10, 2019 07:35 UTC
  • UN: Watu 86 wanaambukizwa Ebola kila wiki DRC

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Dunaini (WHO) limetangaza kuwa kwa wastani watu 86 wanaambukizwa ugonjwa wa Ebola kila wiki nchini Jamhuri ya Kdemokrasia ya Congo, DRC katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri.

Kupitia taarifa yake ya kila wiki, WHO imesema hata hivyo hakuna kisa chochote kilichoripotiwa nje ya DRC.

WHO inasema katika siku 21 zilizopita yaani kuanzia tarehe 17 Julai hadi tarehe 6 mwezi huu wa Agosti wagonjwa wapya 257 waliripotiwa na kuthibitishwa kuwa na Ebola.

Kati yao 116 walitoka mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini, wakifuatiwa na 58 mjini Mandima jimbo la Ituri.

Hata hivyo hakuna mgonjwa aliyeripotiwa kutoka mji wa Goma, tangu ripoti ya awali ambapo kuliripotiwa wagonjwa wanne ambapo kati ya hao wawili walifariki dunia na wengine wawili wanapata matibabu kwenye kituo cha afya cha kutibu Ebola.

Chanjo ya Ebola

Shirika hilo la afya linasema kuwa watu wengine 232 ambao walikuwa na makaribiano na wagonjwa kwenye eneo la Nyiragongo, jimboni Kivu Kaskazini hivi sasa wanafuatiliwa kwa karibu.

Hali kadhalika chanjo dhidi ya Ebola inaendelea kutolewa ikiwemo asilimia 98 ya wanaoshukiwa kuwa karibu na wagonjwa wameshachanjwa.

Hadi tarehe 6 mwezi huu wa Agosti, jumla ya visa 2,781 vimeripotiwa tangu kulipuka kwa ugonjwa huo Kivu Kaskazini mwezi Agosti mwaka jana na kati ya visa hivyo wagonjwa ni 1,866 waliothibitishwa wamefariki dunia.

 

Tags