Uganda: Saudia inawashikilia wanawake 12 raia wetu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5545-uganda_saudia_inawashikilia_wanawake_12_raia_wetu
Bunge la Uganda limearifiwa kuwa wanawake 12 raia wa nchi hiyo wanashikiliwa chini ya mazingira magumu nchini Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 21, 2016 10:53 UTC
  • Uganda: Saudia inawashikilia wanawake 12 raia wetu

Bunge la Uganda limearifiwa kuwa wanawake 12 raia wa nchi hiyo wanashikiliwa chini ya mazingira magumu nchini Saudi Arabia.

Betty Amogi, Mbunge wa Oyam Kusini ameliambia bunge la Uganda kuwa mabinti 12 wa nchi hiyo wanapitia kipindi kigumu baada ya kusafirishwa katika nchi hiyo ya Kiarabu na wakala asiyejulikana na mara baada ya kuwasili, wakapokonywa pasi zao za kusafiria. Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Muungano wa Wabunge Wanawake wa Uganda ameitaka serikali ya Kampala kuingilia kati na kuhakikisha kuwa mabinti hao wanarejeshwa nyumbani mara moja. Mbunge huyo wa Oyam Kusini ameliambia bunge hilo kuwa, miongoni mwa mabinti hao ni Nakamya Latifa, Maku Zamu, Nabukalu Aisha, Kyabaganje Hadija, Nakitta Rebecca, Naigaga Sawiya na Kagoya Sharua miongoni mwa wengine. Rebecca Kadaga, Spika wa Bunge la Uganda naye pia amelieleza bunge hilo kuwa hivi karibuni alipokea simu kutoka kwa mabinti wawili waliodai kuwa wanateseka nchini Saudia, walikokwenda kufanya kazi za ndani. Kadaga ameliambia Bunge hilo kuwa, mabinti hao waliompigia simu wamemuarifu kuwa, mabinti wenzao waliokuwa wamezuiliwa pamoja nao raia wa Kenya na Ghana waliachiwa huru baada ya serikali zao kupitia balozi zao mjini Riyadh kuingilia kati.

Bunge la Uganda limemmtaka Dakta Kamanda Bataringaya, Waziri wa Kazi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki kulishughulikia suala hilo na kuhakikisha kuwa mabinti hao wanarejeshwa nyumbani haraka iwezekanavyo.