Aug 25, 2019 07:55 UTC
  • Boko Haram yaua watu 12 nchini Niger

Wanamgambo wa genge la kigaidi la Boko Haram wameua kwa umati watu 12 wa kijiji kimoja cha kusini mashariki mwa Niger.

Viongozi wa eneo hilo walisema jana kuwa, shambulio hilo la kigaidi lilitokea katika kijiji cha Lamana katika wilaya ya Gueskérou ya jimbo la Diffa lililoko karibu na Ziwa Chad. 

Viongozi wa eneo hilo wamesema kuwa, watu 11 kati ya wanavijiji hao 12 waliouliwa kwa umati, walipigwa risasi. Hata hivyo hawakutoa maelezo zaidi kuhusu wanavijiji wengine. 

Wilaya ya Gueskérou iko karibu na mto wa Komadougou Yobe, unaounda mpaka wa kimaumbile baina ya Niger na Nigeria. Eneo hilo limekuwa uwanja wa mauaji na utekaji nyara watu kwa mika mingi sasa. Mwezi Machi mwaka huu, magaidi wa Boko Haram walifanya mashambulizi mawili kwenye eneo hilo na kuua kigaidi raia wanane na polisi saba.

Magaidi wa Boko Haram wanafanya jinai kubwa dhidi ya binadamu katika nchi nne za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon

 

Kundi la kigaidi la Boko Haram lilibeba silaha na kuanzisha uasi mwaka 2009 kwa lengo la kuasisi utawala eti wa Kiislamu kaskazini mwa Nigeria, ambapo mbali na ndani ya nchi hiyo, limepanua wigo wa mashambulio yake hadi katika nchi jirani za Niger, Chad na Cameroon. Hadi hivi sasa, zaidi ya watu 20 elfu wameshauawa katika nchi hizo nne za magharibi mwa Afrika na zaidi ya wengine milioni mbili wamekuwa wakimbizi. 

Kushindwa nchi za eneo hilo na hasa Nigeria kuliangamiza kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram kama alivyokuwa ameahidi Rais Muhamadu Buhari wa nchi hiyo wakati wa kampeni za uchaguzi, kumedhoofisha mkakati wa kukabiliana na genge hilo.

Tags