Al Shabab 18 wauawa nchini Somalia
Wanachama 18 wa kundi la kigaidi la al Shabab nchini Somalia wakiwemo makamanda wawili wa kundi hilo wameangamizwa katika operesheni ya jeshi la nchi hiyo.
Operesheni hiyo imefanyika katika mkoa wa Shabelle ulioko kusini mashariki mwa Somalia.
Ripoti zinasema kuwa makamanda wawili wa ngazi za juu wa kundi la al Shabab ni miongoni mwa waliouawa katika shambulizi hilo la jeshi la serikali kuu ya Somalia.
Operesheni hiyo ya jeshi la Somalia ilianza miezi kadhaa iliyopita kwa shabaha ya kuyasafisha kabisa maeneo ya kusini mwa nchi hiyo na kuwafurusha wapiganaji wa al Shabab. Kundi la kigaidi lilijiunga na mtandao wa al Qaida mwaka 2012.
Kundi la al Shabab ambalo miaka ya nyuma lilikuwa likidhibiti maeneo ya katikati na kusini mwa Somalia, mwaka 2015 lilipokonywa miji mikubwa ya nchi hiyo na sasa linadhibiti baadhi ya maeneo ya vijijini ya Somalia. Inakadiriwa kuwa kundi hilo sasa lina wapiganaji baina ya elfu 7 hadi 9 nchini Somalia.