Deni la kigeni la serikali ya Misri linazidi kuongezeka
(last modified Tue, 27 Aug 2019 11:54:54 GMT )
Aug 27, 2019 11:54 UTC
  • Deni la kigeni la serikali ya Misri linazidi kuongezeka

Benki Kuu ya Misri imetangaza habari ya kuongezeka deni la kigeni la nchi hiyo na kupindukia dola bilioni 106.

Taarifa hiyo ya Benki Kuu ya Misri imetolewa leo Jumanne na kuongeza kuwa, deni hilo limeongezeka kwa wastani wa dola bilioni 9 na milioni 600 katika kipindi cha miezi minne ya kwanza ya mwaka huu wa 2019 ikilinganishwa na miezi minne ya awali ya mwaka 2018 na sasa deni la kigeni la Misri limefikia dola bilioni 106 na milioni 200.

Katika ripoti yake hiyo, Benki Kuu ya Misri imesema, serikali ya nchi hiyo imechangia dola bilioni 53 katika ongezeko la deni hilo kwenye kipindi cha miezi minne ya awali ya mwaka huu wa 2019, likiwa ni ongezeko la dola bilioni 5 ikilinganishwa na muda kama huo mwaka 2018.

Cairo, mji mkuu wa Misri

 

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, serikali ya Misri imekopa dola bilioni 12 kutoka Mfuko wa Fedha wa Kimataifa IMF na kutekeleza masharti ya mfuko huo kama vile kuwafutia wananchi punguzo la bei ya umeme, kuongeza kodi na ushuru, na kupunguza wafanyakazi serikalini.

Uchumi wa Misri ni uchumi unaolegalega sana. Siasa mbovu za kiuchumi za serikali ya Abdul Fattah el Sisi zimepoelekea kuongezeka ukosefu wa ajira na kupanda kiwango cha umaskini katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Tags