Kesi mpya ya Ebola yagunduliwa nchini Uganda + Sauti
Wizara ya Afya ya Uganda imesema kuwa msichana mmoja mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amepatikana na virusi vya Ebola nchini Uganda. Wizara hiyo imesema kuwa, msichana huyo mwenye umri wa miaka 9, aliwasili nchini Uganda akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ingawa hata hivyo haikumtaja jina lake.
Wizara ya Afya ya Uganda aidha imesema kuwa, msichana huyo aliyegunduliwa kuwa na ugonjwa wa Ebola aliwasili katika eneo la mpakani la Mpondwe, kwenye mpaka wa DRC na Uganda Jumatano wiki hii kutafuta msaada wa matibabu katika mji wa Bwera, Wilayani Kasese, Kusini Magharibi mwa Uganda.
Kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi Agosti 28 nchini DRC, kesi 3004 za maambukizi ya virusi vya Ebola zilikuwa zimeshathibitishwa huko Kongo DR huku watu 1998 wakifariki dunia baada ya kuambukizwa virusi vya Ebola.
Mwandishi wetu wa Kampala Kigozi Ismail na maelezo zaidi