Wanawake wa Somalia wahamasishwa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi wa 2020/2021
Watendaji wa vyombo vya habari vya Somalia na wanaharakati wa haki za binadamu wamekubaliana kufanya kampeni ya kuhamasisha umma juu ya ushiriki wa wanawake katika mchakato wa uchaguzi wa 2020/2021.
Makubaliano hayo yalifikiwa jana mjini Mogadishu katika warsha ya siku moja iliyoandaliwa na Ofisi ya Masuala ya Siasa ya Ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somali (AMISOM) kwa kushirikiana na Kitengo cha Ulinzi, Haki za Binadamu na Masuala ya Jinsia katika kuunga mkono jitihada za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini Somalia (NIEC) za kuzidisha uhamasishaji kuhusiana na mchakatio wa uchaguzi.
Washiriki wa makundi ya vijana, vikundi vya wanawake, wanaharakati wa haki za binadamu na pia waandishi wa habari wa kike wamekubaliana katika warsha hiyo juu ya njia za kutumia ili kukuza ushiriki wa wanawake katika mchakato wa uchaguzi na wa kisiasa nchini Somalia.
Afisa wa masuala ya jinsia wa jumuiya ya Somali Women Free Press Association, Mane Ahmed amesisitiza umuhimu wa wanawake wa Kisomali kupata maarifa ya kutosha juu ya mchakato wa uchaguzi ili waweze kushiriki kikamilifu na kuchangia mchakato huo.
Miongoni mwa masuala muhimu yaliyojadiliwia kwenye warsha hiyo ni pamoja na mafanikio ya yaliyopatikana hivi karibuni katika uwanja huo, usawa wa kijinsia na kuongeza ushiriki wa wanawake katika uchaguzi ujao.