Mavuno mabaya zaidi Somalia tangu 2011, watu milioni 6 wakabiliwa na njaa
Mavuno ya nafaka nchini Somalia mwaka huu wa 2019 yamekuwa ni ya kiwango cha chini zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo tangu mwaka 2011, na hivyo kupelekea watu milioni 6.3 kuhitajia msaada wa dharura wa chakula.
Hayo ni kwa mujibu wa Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, George Conway ambaye amesema sababu kuu ya mavuno duni ni mvua zisizo na mwelekeo wakati wa msimu huo sambamba na kiwango kidogo cha maji kwenye mito.
Takwimu hizo zilizokusanywa na kitengo cha uchambuzi wa uhakika wa chakula na lishe cha shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO na mtandao wa mfumo wa maonyo kuhusu tahadhari ya njaa, FEWNET, zinaonesha kuwa uzalishaji wa nafaka umepungua kwa asilimia 70 chini ya wastani.
Ripoti zinaonesha kuwa kupungua kwa mavuno kumesababisha kuongezeka kwa bei ya mtama wakati wa msimu wa Aprili hadi Juni unaojulikana kama Gu nchini humo.
Kwa kuzingatia hali ya sasa, ripoti zinasema kuwa, “bila usaidizi wa kibinadamu, takribani watu milioni 2.1 nchini Somalia watakabiliwa na njaa hadi mwezi Disemba mwaka huu, na hivyo kufanya idadi ya Wasomali wasio na uhakika wa chakula ifikie milioni 6.3."

Naye Naibu Mwakilishi wa FAO nchini Somalia, Etienne Peterschmit amesema kuwa jambo muhimu ni kutambua kuwa idadi kubwa ya watu wasio na uhakika wa chakula wanaishi vijijini kwa hivyo kuna haja ya kuwezesha watu wazalishe mazao na waweze kuishi kwenye maeneo hayo.
Msimu ujao wa upanzi au Deyr wa kati ya mwezi Oktoba na Desemba unatarajiwa kuwa na kiwango kikubwa cha mvua ambazo maji yake yanatarajiwa kusababisha mafuriko kwenye mito ya Juba na Shabelle na hivyo kuharibu mazao.