Ofisi ya mwanasheria wa Misri yachunguza kifo cha mtoto wa Morsi
(last modified Thu, 05 Sep 2019 11:10:34 GMT )
Sep 05, 2019 11:10 UTC
  • Abdullah Morsi
    Abdullah Morsi

Wakili wa familia ya rais wa zamani wa Misri aliyefariki dunia miezi kadhaa iliyopita akiwa mikononi mwa vyombo vya usalama vya nchi hiyo, Muhammad Morsi amesema kuwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo inafanya uchunguzi kuhusu kifo cha mtoto wa mwisho wa Morsi, Abdullah Morsi aliyeaga dunia ghafla hiyo jana.

Abdel Mon'em Abdel Maqsoud amesema kuwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Misri imeanza uchunguzi huo mapema leo Alkhamisi kutaka kubaini sababu ya kifo cha mtoto wa rais wa zamani wa Misri aliyeondolewa madarakani na kiongozi wa sasa wa nchi hiyo Abdel Fattah al Sisi kupitia mapinduzi ya kijeshi.

Abdullah Morsi aliaga dunia jana ghafla kwa kile kilichosemwa kuwa ni matatizo ya moyo. Maiti yake ilikuwa bado inashikiliwa na vyombo vya usalama kwa uchunguzi zaidi.

Oktoba mwaka jana vyombo vya usalama vya Misri zilimtia nguvuni Abdullah Morsi na kumwachia huru baadaye. Mtoto huyo wa kiume wa rais wa zamani wa Misri pia mwaka 2015 alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na aliachiwa huru baada ya kutumikia kifungo hicho.

Muhammad Morsi alifariki dunia katika mazingira ya kutatanisha

Baada ya Muhammad Morsi kufariki dunia katika mazingira ya kutatanisha akiwa mikononi mwa vyombo vya dola mwezi Juni mwaka huu, Abdullah Morsi aliituhumu serikali ya Cairo kuwa imemuua babaye.

Alisema kuwa vyombo vya usalama vya Misri vilimtaka atie saini hati ya kupokea mwili wa baba yake kabla hata ya kupewa maiti hiyo na akiri kwamba kifo chake kilikuwa cha kawaida. Amesema mazingira yaliyoandamana na kukabidhiwa maiti ya Muhammad Morsi na kuiosha yalikuwa ya kudhalilisha.

Tags