Viongozi wa Ikhwanul Muslimin Misri wahukumiwa vifungo vya maisha jela
Mahakama nchini Misri imewahukumu viongozi kadhaa wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin vifungo vya maisha jela.
Kwa mujibu wa taarifa, katika hukumu ambazo zilitolewa Jumamosi, Mohammad Badie kiongozi wa ngazi za juu wa Ikhwanul Muslimin pamoja na wenzake 10 wamehukumiwa kifungo cha maisha gerezani. Huko nyuma pia Badie aliwahi kupatikana na hatia kwa makosa mengine na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Kati ya wanachama wengine waandamizi ambao wamehukumiwa kifungo cha maisha jela ni pamoja na Rashad Bayumi, Saad El-Katatni, Essam el-Erian na Mohamed Beltagy.
Aidha mahakama ya Misri imewahukumu kifungo cha miaka 15 gerezani wanachama wengine wa Ikhwanul Muslimin.
Itakumbukwa kuwa, Rais halali wa Misri Muhammad Morsi, wa harakati ya Ikwanul Muslimin alipinduliwa na jeshi mwaka 2013 na nafasi yake kuchukuliwa na Rais wa sasa Abdel Fattah al Sisi. Rais huyo wa zamani wa Misri alifariki dunia kwa mshituko wa moyo akiwa anahudumia kifungo cha maisha gerezani.
Hivi sasa El Sisi wa Misri anasisitiza kuhusu kukandamizwa Ikhwanul Muslimin kwa visingizio kama vile kuhusika harakati hiyo na vitendo vya misimamo mikali ya kidini. Tayari serikali ya Misri imeitangaza Harakati ya Ikwanul Muslimin kuwa kundi la kigaidi.