Wasichana waliotekwa na Boko Haram, kisingizio cha propaganda za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5611-wasichana_waliotekwa_na_boko_haram_kisingizio_cha_propaganda_za_marekani
Mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesisitiza udharura wa kufuatiliwa hatima ya wasichana waliotekwa nyara na kundi la Boko Haram nchini Nigeria.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 23, 2016 04:19 UTC
  • Wasichana waliotekwa na Boko Haram, kisingizio cha propaganda za Marekani

Mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesisitiza udharura wa kufuatiliwa hatima ya wasichana waliotekwa nyara na kundi la Boko Haram nchini Nigeria.

Samantha Power aliyasema hayo jana alipokutana na wanaharakati wanaofuatilia hatma ya wasichana hao wanaoendelea kushikiliwa na wapiganaji wa kundi hilo la kigaidi nchini Nigeria na kuongeza kuwa, mbali na ushirikiano wa Marekani na Nigeria katika uga wa kupambana na ugaidi wa Boko Haram, nchi mbili hizo zitashirikiana pia katika sekta za kibiashara, kiuchumi na kuimarisha asasi za serikali na kupambana na ufisadi. Ameongeza kuwa, intelijensia ya Washington na pia ushirikiano mzuri uliopo kati ya serikali ya Nigeria na Marekani, utasaidia kupatikana kwa wasichana hao.

Matamshi hayo ya balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa yametolewa huku ikiwa imepita miaka miwili tangu wasichana hao watekwe nyara lakini Washington haijachukua hatua yoyote ya maana katika uwanja huo.

Itakumbukwa kuwa, tarehe 14 April mwaka 2014, wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram waliwateka nyara wasichana 276 waliokuwa wakisoma shule ya sekondari ya Chibok katika jimbo la Borno na kwenda nao kusikojulikana. Baadhi ya wasichana hao walifanikiwa kutoroka kutoka mikononi mwa magaidi hao na hatima ya wengine 219 haijulikani hadi sasa. Kundi la Boko Haram lilidai kuwa sababu ya kuwateka nyara wasichana hao ni kuwazuia kupata elimu ya Kimagharibi. Kundi hilo la kigaidi linaamini kuwa, ni haramu kusoma elimu ya Magharibi.

Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, japokuwa fikra za walimwengu ziliathiriwa sana na tukio hilo lakini inaonekana kuwa, viongozi wa nchi za Magharibi na Nigeia yenyewe badala ya kuelekeza jitihada zao katika kuwatafuta wasichana hao, wanatumia tukio hilo kwa malengo ya kisiasa na kipropaganda. Katika kampeni zake za uchaguzi, Rais Muhammadu Buhari aliahidi kuwatafuta na kuwarejesha wasichana hao katika familia zao, kuliangamiza kundi la Boko Haram na kurejesha amani huko kaskazini mwa Nigeria. Hata hivyo hadi sasa kiongozi huyo hajatimiza ahadi zake kwa Wanigeria.

Baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wanalituhumu jeshi la Nigeria kwamba halifanyi jitihada za kutosha za kuwakomboa wasichana hao na kwamba linatumia maudhui hiyo katika propaganda za kupata misaada ya kijeshi. Rais Buhari ambaye alikuwa na matumaini makubwa kwa misaada ya silaha ya Marekani, katika safari yake ya kwanza nchini humo alirudi mikono mitupu baada ya kukataliwa misaada ya serikali ya Washington, suala ambalo kwa mara nyingine tena limethibitisha uongo wa madai ya Marekani eti ya kupambana na ugaidi.

kwa sasa Marekani inatoa nara ya kuwakomboa wasichana wa Nigeria waliotekwa nyara na kundi la Boko Haram huku wachambuzi wa mambo wakiisuta Washington kwamba imekuwa na mchango mkubwa katika kuanzisha makundi ya kigaidi na kuyasaidia kwa silaha na fedha.

Wiki iliyopita katika kumbukumbu ya mwaka wa pili tangu wasichana hao watekwe nyara, maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa walitoa taarifa wakitaka kuzidishwa jitihada za kuwakomboa wasichana hao.

Wakati huo huo ripoti za taasisi za kimataifa zinasisitiza kuwa, idadi kubwa ya wasichana hao wamebakwa na kunajisiwa, wengine wameuzwa kama watumwa na baadhi yao wanatumiwa katika mashambulizi ya kijilipua kwa mabomu yanayofanywa na kundi la Boko Haram katika maeneo mbalimbali.

Kwa kutilia maanani hali hiyo, matamshi ya balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa na ahadi zake za misaada na ushirikiano katika kupambana na kundi la kigaidi la Boko Haram na kuwakomboa wasichana hao zinaonesha tena siasa na sera za kinafiki na kindumakuwili za serikali ya Washington.