Watu 14 wauawa katika shambulio la waasi kaskazini mashariki mwa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56115-watu_14_wauawa_katika_shambulio_la_waasi_kaskazini_mashariki_mwa_drc
Viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamesema kuwa, watu 14 wameuawa katika shambulio la kundi moja la waasi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Sep 19, 2019 10:04 UTC
  • Watu 14 wauawa katika shambulio la waasi kaskazini mashariki mwa DRC

Viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamesema kuwa, watu 14 wameuawa katika shambulio la kundi moja la waasi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Charité Banza, mkuu wa asasi ya kijamii ya eneo la Djugu mkoani Ituri, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema kuwa, kundi la waasi jana Jumatano lilivamia kijiji cha DAR katika eneo hilo na kuua raia 14 na kujeruhi wengine wanne.

Banza ameongeza kuwa, jeshi la Kongo kimsingi haliko kwenye eneo hilo hivyo lilishindwa kukabiliana na waasi hao.

Mkuu huyo wa asasi ya kijamii wa eneo la Djugu amesema kuwa, usalama katika jimbo la Ituri ni mdogo sana na kila siku watu wasio na hatia wanauawa bila sababu.

 

Kwa upande wake Jules Ngongo, msemaji wa jeshi la Kongo katika jimbo la Ituri amethibitisha kutokea shambulio hilo lakini amekataa kutoa maelezo zaidi.

Kwa muda wa miaka 20 sasa maeneo ya mashariki na katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hayana usalama, huku makundi yenye silaha yakichomoza kama uyoga.

Mbali na usalama mdogo, maeneo hayo ya Kongo yanasumbuliwa pia na matatizo mengine mengi yakiwemo ya maradhi ya kuambukiza, hasa ugonjwa hatari wa Ebola.

Jeshi la Kongo na hata askari wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani wameshindwa kuwadhaminia wakazi wa maeneo hayo usalama wao jambo ambalo limezidi kuyafanya maeneo hayo yasiwe na utulivu wa aina yoyote ile kwa zaidi ya miongo miwili sasa.