Mamia ya Wanigeria wamerejea nyumbani wakihofia mashambulizi ya xenophobia
Maafisa wa serikali ya Nigeria wametangaza kuwa raia zaidi ya 300 wa nchi hiyo wamerejea nyumbani hadi sasa kutoka Afrika Kusini kwa kuhofia mashambulizi yanayowalenga raia wa nchi za Kiafrika wanaoishi nchini humo.
Kundi la pili la Wanigeria 314 kutoka Afrika Kusini liliwasili Lagos Jumatano ya juzi wakikimbia mauaji na hujuma zinazowalenga Waafrika wanaofanyakazi au kuishi nchini humo.
Ukatili na mashambulizi ya sasa dhidi ya raia wa kigeni nchini Afrika Kusini yameua watu 12 kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu wa Septemba.
Nigeria, baina ya nchi za Afrika, ndiyo yenye idadi kubwa ya raia nchini Afrika Kusini ambao ndio walioathirika zaidi kwa hujuma na mashambulizi hayo.
Siku mbili zilizopita Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini alituma wajumbe katika nchi kadhaa za Kiafrika ambazo raia wake waliathirika zaidi na hujuma na mashambulio ya chuki dhidi ya raia wa kigeni kutoka Afrika akiziomba radhi serikali na wananchi wa nchi hizo.

Khusela Diko, msemaji wa serikali ya Afrika Kusini amesema kuwa, Rais Ramaphosa ametuma wajumbe katika nchi za Niger, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Tanzania, Nigeria, Zambia, Ghana na Senegal.
Wiki iliyopita, Rais Ramaphosa alinukuliwa na duru za habari akisema kuwa, anaona aibu kwa matukio ya kushambuliwa raia wa kigeni Waafrika katika nchi yake.