Wamisri wafanya maandamano dhidi ya utawala wa Rais Sisi
(last modified Sat, 21 Sep 2019 07:14:21 GMT )
Sep 21, 2019 07:14 UTC
  • Wamisri wafanya maandamano dhidi ya utawala wa Rais Sisi

Wananchi wa Misri wamefanya maandamano dhidi ya Rais Abdel Fattah al-Sisi wa nchi hiyo.

Maandamano hayo dhidi ya utawala wa Sisi yamefanyika usiku wa kuamkia leo katika mji mkuu na Cairo na miji mingine mikubwa ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Ni nadra sana maandamano ya aina hii kushuhudiwa nchini Misri katika utawala huu wa Sisi.

Baadhi ya waandamanaji walikuwa wamebeba mabango yaliyokuwa na jumbe za kukosoa ufisadi wa utawala wa Sisi, huku wengine wakisikika wakipiga nara zinazosema "Sisi Ondoka".

Maafisa usalama wametumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuzima maandamano hayo. Aidha watu kadhaa walioshiriki maandamano hayo wametiwa mabaroni.

Hii ni katika hali ambayo, serikali ya al-Sisi imekuwa ikikosolewa kwa kuwakandamiza wapinzani na hasa viongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin sambamba na kuviwekea mbinyo vyombo vya habari, tangu kiongozi huyo ashike hatamu za uongozi kupitia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2013.

Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri akitokwa na kijasho

Aprili mwaka huu, wananchi wa Misri walishiriki kura ya maoni, iliyokuwa na azma ya kuondoa kikomo cha muhula wa rais, hatua ambayo inamruhusu Rais Abdulfattah al-Sisi wa nchi hiyo kugombea zaidi ya mihula miwili inayoruhusiwa na katiba.

Kabla ya hapo, Bunge la Misri lilipasisha muswada unaoruhusu kukifanyia marekebisho kipengee cha 140 cha katiba, ambacho kinasema rais anapaswa kugombea mihula miwili pekee ya miaka minne minne, na hivyo kumuandalia mazingira Sisi ya kubakia madarakani hadi mwaka 2030.

 

Tags