Waandamanaji zaidi ya 650 watiwa mbaroni Misri
Vyombo vya sheria vya Misri vimewatia mbaroni wafanya maandamano zaidi ya 650. Watu hao walikuwa wakiandamana dhidi ya serikali ya Rais Abdel Fattah al Sisi.
Kuendelea maandamano ya siku tatu dhidi ya Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri kumepelekea askari usalama na polisi wa nchi hiyo kuvamia nyumba za wafanya maandamano baada ya kutambua utambulisho wao; na kwa mujibu wa vyombo vya sheria, hadi sasa watu zaidi ya 650 wametiwa mbaroni na kutupwa jela.
Wafanya maandamano nchini Misri wamekuwa wakiandamana kwa siku ya tatu sasa katika mitaa ya mji mkuu Cairo na khususan katika medani ya At-Tahrir na medani nyinginezo nchini humo wakilalamikia ufisadi wa serikali. Wafanya maandamano hao wametaka kujiuzulu Rais Abdel Fattah al Sisi. Al Sisi aliingia madarakani Misri mwaka 2014. Maandamano dhidi ya Rais huyo wa Misri yalianza tangu Ijumaa iliyopita na yanatazamiwa kuendelea pia katika siku zijazo kufautia wito wa vyama vya kisiasa nchini humo.