Makumi ya watu waliotekwa nyara Nigeria waachiwa huru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56213-makumi_ya_watu_waliotekwa_nyara_nigeria_waachiwa_huru
Makumi ya watu waliokuwa wametekwa nyara na watu wenye silaha kaskazini magharibi mwa nchi ya Nigeria kwa miezi kadhaa sasa hatimaye wameachiwa huru.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 24, 2019 04:40 UTC
  • Makumi ya watu waliotekwa nyara Nigeria waachiwa huru

Makumi ya watu waliokuwa wametekwa nyara na watu wenye silaha kaskazini magharibi mwa nchi ya Nigeria kwa miezi kadhaa sasa hatimaye wameachiwa huru.

Msemaji wa Gavana wa jimbo la Zamfara, Abubakar Dauran amewaambia wanahabari kwamba, miongoni mwa walioachiwa huru ni watoto wa kike 16.

Watu hao 31 walioachiliwa huru walikuwa wameshikiliwa mateka na genge la wabeba silaha kwa muda wa miezi minane. Haijabainika iwapo kundi hilo lina mfungamano wowote na genge la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.

Mapigano ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji hutokea katika eneo hilo la kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Makundi yenye silaha yamekuwa yakishambuliana na kushika watu mateka hususan katika maeneo ya kaskazini na mashariki mwa Nigeria.

Wasichana wa Shule ya Chiboka baada ya kuachiwa huru na Boko Haram

Mwishoni mwa mwezi uliopita, watu wasiojulikana waliwateka nyara raia wasiopungua 50 katika shambulizi walilolifanya kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Wananchi wa Nigeria wanaamini kuwa kushindwa serikali ya Abuja kuwadhaminia usalama kunapelekea kuongezeka mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram na magenge ya wabeba silaha, na ndio maana eneo la kaskazini magharibi limekuwa likishuhudia machafuko na vitendo vya uhalifu mara kwa mara.